Na Stella Herman, Shinyanga
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga imezindua rasmi Klabu ya Kodi (Tax Club) katika Shule ya Sekondari Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu umuhimu wa kodi, wajibu wa kulipa kodi na mchango wa kodi katika maendeleo ya taifa.
Uzinduzi huo umefanyika leo Oktoba 2,2026 katika Shule ya Sekondari Shinyanga, ambapo Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Maro, amewataka wanafunzi kutumia fursa hiyo kujenga misingi ya uadilifu, nidhamu, uzalendo, ubunifu na moyo wa ujasiriamali.
Maro amesema wanafunzi kupitia Tax Club hiyo wanapaswa kujifunza na kuelewa sheria za kodi, huku wakitambua kuwa elimu wanayoipata inaweza kuwasaidia kuwa raia wenye uelewa wa wajibu wao kwa taifa.
Amesema Tax Club pia inatoa fursa kwa wanafunzi kuwa sehemu ya juhudi za kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kodi.
“Kupitia Tax Club hii, nendeni mkasimamie na kuiwezesha kodi iweze kufanya kazi yake inayotegemewa,” amesema Maro
Baadhi ya wanafunzi wa Tax Club ya Shule ya Sekondari Shinyanga wameeleza kuwa kuanzishwa kwa klabu hiyo kutawasaidia kuongeza uelewa kuhusu kodi na namna inavyohusiana na maendeleo ya nchi.
Andrew Gati mwanafunzi wa Tax Club Shinyanga Sekondari, amesema klabu hiyo itawapa fursa ya kujifunza zaidi kuhusu kodi na kuwafikishia wengine elimu watakayoipata.
Naye Fred Joshua, mwanafunzi wa Tax Club Shinyanga Sekondari amesema klabu hiyo itawasaidia wanafunzi kuelewa kwa undani masuala ya kodi na wajibu wao kama vijana katika kujenga taifa.
Kwa kuanzishwa kwa Tax Club hiyo, wanafunzi wanatarajiwa kuwa sehemu ya kizazi kinachopata elimu ya kodi mapema na kushiriki katika kuhamasisha uelewa wa masuala ya kodi miongoni mwa vijana na jamii kwa ujumla.
Akitoa elimu ya kodi kwa wanachama wa Tax Club hiyo, Afisa Msimamizi wa Elimu kwa Mlipa Kodi, Semeni Mbeshi, amesema wanafunzi wana nafasi muhimu ya kusaidia Serikali kwa kuwafikishia vijana wengine elimu kuhusu kodi.
Mbeshi amesema wanafunzi wanapaswa kutumia maarifa watakayoyapata kupitia klabu hiyo kuwaelimisha wenzao kuhusu umuhimu wa kodi na wajibu wa wananchi kufuata sheria na taratibu za kodi.
Amesema kupitia Tax Club, wanafunzi wataweza kupata uelewa wa mapema kuhusu masuala ya kodi ambao utakuwa msingi muhimu wanapokuwa watu wazima na kuanza kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Social Plugin