Na mwandishi wetu,Pwani
Kituo cha Uhakiki wa Vipimo kinachomilikiwa na Wakala wa Vipimo (WMA) cha Misugusu mkoani Pwani kimeongeza uwezo wa kuhakiki magari yanayosafirisha mafuta kutoka magari nane hadi 60 kwa siku, hatua inayowarahisishia wafanyabiashara na wasafirishaji kupata huduma kwa wakati.
Meneja wa kituo hicho, Mrisho Mandari, amesema kazi kubwa ya kituo ni kuhakiki magari yanayosafirisha mafuta ya petroli na dizeli kutoka Tanzania na nchi jirani, zikiwemo Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Burundi.
Mandari amesema awali huduma hizo zilitolewa katika kituo cha Ilala, ambacho kilikuwa na uwezo wa kuhakiki magari manane kwa siku. Hata hivyo, Serikali ilijenga kituo kipya cha Misugusu ili kuongeza uwezo wa kuhudumia wateja na kupunguza muda wa kusubiri.
Amesema kwa sasa kituo kina uwezo wa kuhakiki magari 60 kwa siku, hivyo kuwawezesha wasafirishaji kutoka mikoa mbalimbali kufika, kupata huduma na kuendelea na shughuli zao bila usumbufu mkubwa.
Raymond George kutoka Kampuni ya Abood Morogoro amesema ameridhishwa na huduma alizopata baada ya kufika kituoni hapo asubuhi na kukamilisha zoezi la uhakiki siku hiyo hiyo. Amewahimiza wasafirishaji wengine kutoka mikoani kutumia kituo hicho ili kurahisisha shughuli zao.
Kwa upande wake, Anthony Mulenga kutoka Zambia, anayefanya kazi katika Kampuni ya Latitude, amesema kampuni yao hupeleka magari yale Tanzania kwa ajili ya uhakiki wa vipimo. Amesema wamekuwa wakipata huduma nzuri na kwamba madereva wao hawajawasilisha malalamiko kuhusu huduma wanazopata kituoni hapo.
Baadhi ya wateja wengine wameeleza kuridhishwa na muda unaotumika kukamilisha uhakiki, wakisema hurudi kituoni baada ya muda wa vyeti vyao vya uhakiki kuisha ili kufanya ukaguzi unaohitajika na kuendelea na shughuli za usafirishaji.


Social Plugin