Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA BUNGE YA TAMISEMI YATAKA WAFANYABIASHARA WA ZAMANI KUPEWA KIPAUMBELE KWENYE MIRADI YA MAENDELEO, KAHAMA






Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Florent Kyombo, akizungumza wakati kamati hiyo ilipotembelea kuona na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo Manispaa ya Kahama, ikiwemo jengo la mama na mtoto pamoja na miradi ya Tactic.

Na Neema Nkumbi - KAHAMA

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Florent Kyombo, ameielekeza Manispaa ya Kahama kuhakikisha wafanyabiashara waliokuwa wakifanya shughuli zao katika maeneo yanayojengwa upya, wanapewa kipaumbele katika masoko na vituo vipya vya biashara.

Kyombo amesisitiza upangishaji wa bei rafiki kwa wajasiriamali wa maeneo hao ili kutoa fursa kwa kila mmoja kufanya shughuli za kujiingizia kipato.

Ametoa wito huo wakati wa ziara ya kamati hiyo, iliyokagua miradi sita ya maendeleo katika Manispaa ya Kahama, akieleza kuwa uwekezaji huo unapaswa kuwanufaisha wananchi waliokuwa wakitegemea maeneo hayo kwa shughuli zao za kiuchumi.

“Kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, miradi hii wakati inajengwa kuna wananhi ambao walikuwa wanatoa huduma katika mazingira ambayo hayakuwa katika kiwango kile kinachotakiwa, tunaomba viongozi wetu wa mkoa na wilaya, tuhakikishe kwamba wale wenyeji wa maeneo yote wanapewa kipaumbele waweze kuendeleza shughuli zao za kiuchumi”,amesema.

Sambamba na hilo amesisitza viongozi wa Manispaa kusimamia gharama za upangishaji katika masoko na vituo vya mabasi zinaendana na uwezo wa wafanyabiashara, ili miundombinu inayojengwa isiwatenge wananchi ambao wamekuwa wakijipatia kipato kupitia shughuli hizo.

“Tunaendelea kuwasihi kuhusu bei za kupangisha katika maeneo yetu ziwe bei rafiki kwa wananchi na wajasiriamali wote wanaojitafutia kipato katika maeneo hayo”, amesema Kyombo.

Amesema wastani wa utekelezaji wa miradi iliyokaguliwa umefikia asilimia 61, akiwataka viongozi, wakandarasi na washauri elekezi kuongeza kasi ya kazi ili miradi ikamilike kwa wakati na wananchi waanze kunufaika na huduma zake.

“Wananchi wanataka matokea, wanataka kuona mirdi hii imekamilika, kwa hiyo tunaamini ndani ya kipindi hiki cha mkataba mtamaliza, tukirudi wakati mwingine tukute miradi hii imekamilika. TAMISEMI, naibu katibu mkuu tunaomba fedha tukamilishe”,amesema.

TAMISEMI YAHIDI FEDHA ZA MIRADI

Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, John Cheyo, amesema Serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Kahama, akiwahakikishia wakandarasi kuwa fedha za kuwalipa zipo.

“Naomba niseme tu kwamba fedha kwa ajili ya kuwalipa wakandarasi wetu zipo, wakandarasi wanaofanya vizuri tupo nao sambamba na tunatambua michango yao” ,amesema Cheyo.

Kuhusu wafanyabiashara waliokuwa katika eneo la soko kabla ya ujenzi, Cheyo amesema watapewa kipaumbele kurejea katika maeneo hayo.

“Tutahakikisha wafanyabiashara walioondoka katika maeneo yao kupisha ujenzi, watapewa kipaumbele kurejeshwa kwenye maeneo yao. Kwa wengine sasa tutasimamia taratibu zingine ziendelee”,amesema.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Pili Mnyema, amesema uwekezaji wa miradi ya kimkakati unaofanywa na Serikali mkoani humo, unalenga kuinua uchumi wa Shinyanga, hivyo kwa kushirikiana na halmashauri, watahakikisha utekelezaji wake unakuwa wa viwango vinavyotakiwa.

“Tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba miradi yote inayoendelea inakamilika kwa wakati, kuna miradi mingi ya kimkakati, kwa sababu dhamira na nia njema ya Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha mkoa wa Shinyanga unainuka kiuchumi, tupo tayari kuendelea kuisimamia”, amesema Mnyema.

NGAYIWA ATAKA WANANCHI WAPEWE NAFASI

Mbunge wa Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, amesema ugawaji wa maeneo haupaswi kufuata misingi ya vyama vya siasa, bali kuzingatia maslahi ya wananchi na fursa za kiuchumi zinazotokana na uwekezaji huo.

Aidha, ameitaka Serikali kuendelea kutoa fedha kwa wakati ili mradi ukamilike haraka na wananchi waanze kunufaika na huduma zinazotarajiwa.

MASINDI AWATAKA WAWEKEZAJI KUMIMINIKA KAHA​MA

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi, anayekaimu Wilaya ya Kahama, amewataka wawekezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania kutumia fursa za kiuchumi zilizopo Kahama, akieleza kuwa mazingira ya kukuza biashara na uzalishaji ni rafiki.

Amesisitiza kuwa fursa za uwekezaji Kahama zinapaswa kutumiwa kuongeza uzalishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi, huku akieleza kuwa maendeleo ya eneo hilo yanahitaji ushiriki wa Serikali, sekta binafsi na wananchi wenyewe.

“Kahama milango ya kiuchumi imefunguliwa saa 24, watanzania njooni muwekeze Kahama, tunahitaji wawekezaji watakaochukua fursa za kuzalisha kutoka maeneo mengine wazilete hapa”, amesema Masindi.

Ameipongeza Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji unaofanyika, huku akiwataka wananchi kutunza miundombinu hiyo ili iendelee kutoa huduma kwa muda mrefu.








































Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com