Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HATUA BOND YAVUNJA REKODI, YAKUSANYA SHILINGI BILIONI 161.38


-Hatifungani ya I&M Bank yazidi lengo kwa asilimia 806.92
-wawekezaji wa ndani waongoza kwa ushiriki


Hatifungani ya Hatua Bond iliyotolewa na I&M Bank Limited imeweka rekodi mpya katika soko la mitaji nchini baada ya kukusanya shilingi bilioni 161.38, sawa na asilimia 806.92 ya lengo la awali la kukusanya shilingi bilioni 20.


Mafanikio hayo yameifanya Hatua Bond kuwa miongoni mwa hatifungani za kampuni zilizopata mafanikio makubwa zaidi nchini, ikivunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na iTrust Bond ya iTrust Finance Limited, iliyokusanya shilingi bilioni 114.12, sawa na asilimia 760.78 ya lengo lake.

Akizungumza leo, Oktoba 15, 2026, jijini Dar es Salaam, katika hafla ya kuorodheshwa kwa Hatua Bond kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, amesema mafanikio hayo ni hatua muhimu katika maendeleo ya masoko ya mitaji nchini.

Amesema Hatua Bond imeweka rekodi nyingine kwa kuwa mauzo ya toleo lake la kwanza yamezidi thamani ya programu nzima ya hatifungani ya I&M Bank, iliyopangwa kukusanya shilingi bilioni 100 kupitia awamu nne kati ya mwaka 2026 na 2029.

“Naipongeza I&M Bank Limited pamoja na iTrust Finance Limited, ambao walikuwa washauri wakuu elekezi wa muamala huo, pamoja na taasisi nyingine zilizoshiriki kufanikisha utoaji na uorodheshwaji wa hatifungani hiyo,” amesema CPA. Mkama.


Amesema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 95.48 ya wawekezaji walioshiriki katika Hatua Bond ni wawekezaji binafsi, huku asilimia 4.52 wakiwa kampuni na taasisi. Aidha, asilimia 95.73 ya wawekezaji ni wa ndani ya nchi, wakati asilimia 4.27 ni wawekezaji wa kigeni.


"Ushiriki mkubwa wa wawekezaji binafsi wa ndani, unaonesha kuongezeka kwa mwitikio wa wananchi katika kutumia fursa za uwekezaji zinazopatikana kwenye masoko rasmi ya fedha'',amesema CPA.Mkama


Amesema kuwa mafanikio hayo yamechangiwa pia na mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kiutendaji yanayowekwa na Serikali, yakiwamo vivutio vya kikodi katika hatifungani za kampuni na taasisi, kupunguza kiwango cha chini cha uwekezaji na kuboresha utaratibu wa malipo ya riba.

Amebainisha kuwa katika Hatua Bond, kiwango cha chini cha uwekezaji kilipunguzwa kutoka shilingi milioni moja hadi shilingi 500,000 kwa idhini ya CMSA, hatua inayopanua fursa kwa wawekezaji wadogo, wakiwamo vijana na wanawake.


Vilevile, malipo ya riba yanafanyika kila baada ya miezi mitatu badala ya miezi sita, hali inayowawezesha wawekezaji kupokea mapato yao mara nyingi zaidi ndani ya mwaka.


Amesema CMSA imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu fursa na faida za uwekezaji katika masoko ya mitaji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza ushiriki wa wananchi katika sekta rasmi ya fedha.

Ameongeza kuwa mafanikio ya Hatua Bond yanaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi shindani, himilivu na jumuishi kwa maendeleo endelevu ya nchi.


CPA.Mkama amesema kuorodheshwa kwa Hatua Bond katika DSE kumeongeza thamani ya uwekezaji katika hatifungani za kampuni na taasisi kwa asilimia 4.48, kutoka shilingi trilioni 2.23 hadi shilingi trilioni 2.33.

Ameeleza kuwa kuorodheshwa huko pia kunatoa fursa kwa wawekezaji kuuza hatifungani zao wanapohitaji fedha na kuwawezesha wawekezaji wapya kuingia sokoni. Hatua hiyo pia inachangia kuongeza ukwasi na kuwezesha upatikanaji wa taarifa za thamani ya hatifungani sokoni.


Akihitimisha hotuba yake, CPA.Mkama amezitaka kampuni na taasisi za sekta ya umma na binafsi kutumia fursa zinazotolewa na masoko ya mitaji kupata fedha kwa ajili ya kukuza biashara na kugharamia miradi ya maendeleo.

Pia, amezitaka kampuni zenye leseni za kutoa huduma katika masoko ya mitaji kuendelea kubuni bidhaa zitakazopanua fursa za uwekezaji kwa wananchi na wawekezaji wa kimataifa.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com