
Mbunge wa jimbo la Bukoba Eng. Johnston Johansen Mutasingwa akiwa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mh. Erasto Siima wakikabidhi jezi na mpira kwa timu ya Mpira wa miguu.


Mbunge wa jimbo la Bukoba Eng. Johnston Johansen Mutasingwa akiwa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mh. Erasto Siima wakikabidhi jezi na mpira kwa timu ya Mpira wa pete.


Mbunge wa jimbo la Bukoba Eng. Johnston Johansen Mutasingwa akizungumza



Na Mbuke Shilagi - Kagera.
Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Mhandisi Johnston Johansen Mutasingwa, ameendelea kuhamasisha na kuimarisha michezo kwa vijana baada ya kukabidhi jezi na mipira kwa jumla ya timu 34 katika kata tatu za Manispaa ya Bukoba.
Timu 30 za mpira wa miguu pamoja na timu nne za mpira wa pete zimepokea vifaa hivyo katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Kaitaba, ikiwa ni awamu ya pili ya ugawaji wa vifaa vya michezo unaotekelezwa na Mbunge huyo.
Mhandisi Mutasingwa amesema lengo la mpango huo ni kuwaunganisha vijana kupitia michezo, kuwapatia vifaa vya mazoezi na kuwafanya watumie muda wao katika shughuli zenye manufaa badala ya kujihusisha na mambo yasiyofaa.
Amesema mpango wa ugawaji wa vifaa unaendelea hadi timu zote zilizopo katika kata 14 za Jimbo la Bukoba Mjini zinapata jezi na vifaa vya michezo.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mhe. Erasto Siima, ambapo amewataka vijana kutunza amani, akieleza kuwa shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanyika katika jamii zinategemea uwepo wa amani.
Mhe. Siima ameongeza kuwa ushirikiano unaoonekana katika shughuli mbalimbali, ikiwemo usafi unaofanyika kwa pamoja katika kata kila Jumamosi, unatokana na mazingira ya amani yaliyopo.
Kwa upande wake, Mhandisi Mutasingwa amewataka vijana kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali, ikiwemo mikopo, ili kujiajiri na kuanzisha shughuli za kiuchumi zitakazowasaidia kujenga maisha yao.
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Bukoba, Mhe. Shabani Mdoe, amewataka viongozi kusimamia na kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Mhe. Mdoe amesema vifaa hivyo vinatolewa kwa lengo la kuwasaidia vijana kushiriki katika michezo mbalimbali na kufanya mazoezi, hivyo viongozi wanapaswa kuhakikisha vinatumika ipasavyo na vinaendelea kuwa na manufaa kwa vijana.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi, madiwani, Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na viongozi wengine wa serikali na chama.
Zoezi hilo ni sehemu ya mpango wa kuendeleza michezo, kuibua vipaji na kuwaunganisha vijana katika Jimbo la Bukoba Mjini, huku ugawaji wa vifaa ukiendelea hadi timu za kata zote 14 za Bukoba Mjini zitakapofikiwa.



Social Plugin