Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC MASINDI APELEKA UTATUZI KERO ZA WANANCHI MWASUBI


Na Sumai Salum-Kishapu


MKUU wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Mwasubi, ukiwakutanisha wananchi wa Vijiji vya Mwasubi, Itongoitale na Ngw’anghili, ambapo amesikiliza changamoto mbalimbali ikiwemo maji, barabara, elimu na huduma za afya.


Mkutano huo umefanyika Oktoba 8, 2026 katika Kijiji cha Ngw’anghili, ambapo wananchi wamewasilisha changamoto ya huduma ya maji pamoja na ubovu wa barabara ya Mwanamakanga–Ngw’ang’hili, huku wakieleza pia hitaji la kuwa na Shule ya Sekondari ya Kata ili wanafunzi wasilazimike kusoma katika Shule ya Sekondari Bunambiyu.


Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Masindi amesema mafanikio ya mwanadamu yamebebwa na mambo manne, ambayo ni kumjua Mungu kwa kuwa ndiye mtoa baraka na neema, kuwa na ushirika na watu, kufanya kazi kwa bidii pamoja na kujali muda, akiwataka wananchi kuzingatia misingi hiyo katika maisha yao ya kila siku.


Kuhusu changamoto ya maji, Mha. Masindi amewasiliana kwa njia ya simu na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kishapu, Mhandisi Dickson Kamazima, ambaye amesema Tanzania ina jumla ya vijiji 575 ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya maji, huku Wilaya ya Kishapu ikiwa na vijiji 42. Amesema kupitia Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria, kwa mwaka huu vijiji vitatu vimeanza kunufaika, ambavyo ni Itongoitale Kata ya Mwasubi, Wizunza Kata ya Mwadui Lohumbo na Mihama Kata ya Lagana.


Mhandisi Kamazima amesema wakati wananchi wakisubiri utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria ambao unatarajiwa kuchukua muda, wataalamu wa survey kutoka Bonde la Kati wameingia Kijiji cha Itongoitale kwa ajili ya kutafuta chanzo cha maji, na baadaye wataendelea na Kijiji cha Ngw’anghili.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Mwasubi wilayani humo wa kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili mnamo Oktoba 8, 2026 katika Kijiji cha Ngw’anghili


Akizungumza kuhusu barabara ya Mwanamakanga–Ngw’ang’hili, Meneja wa TARURA Wilaya ya Kishapu, Mha. Eliya Mgaya, amesema ni kweli barabara hiyo imeharibika kwa kiasi kikubwa, huku akieleza kuwa mipango ipo katika taratibu za manunuzi ya awamu ya pili inayotarajiwa kuanza mwezi Desemba 2026. Amesema ukarabati utafanyika katika maeneo yenye changamoto kubwa kwa kuweka vifusi na mawe ili kurejesha hali ya barabara hiyo.


Mkuu wa Wilaya ameitaka TARURA kuhakikisha barabara hiyo haigeuki kuwa kikwazo kwa wananchi wanaoitumia, akieleza kuwa ni muhimu kwa usafirishaji wa mazao na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.


Diwani wa Kata ya Mwasubi, Mhe. Samson Gelewa, amesema Serikali tayari imeipatia Kata hiyo kiasi cha Sh milioni 603 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata katika Kijiji cha Ngw’ang’hili, fedha ambazo zitatumika kujenga vyumba nane vya madarasa, matundu 11 ya vyoo, jengo la utawala, jengo la TEHAMA na maabara.


Mhe. Gelewa amesema wananchi pia wameendelea kushiriki katika ujenzi wa huduma za afya kwa kujenga boma la zahanati, huku Ofisi ya Mbunge ikiwawezesha kwa kutoa mbao 100 na mabati 70 kwa ajili ya upauaji wa jengo moja. Amesema wananchi wamechangia fedha za kumlipa fundi, wakati Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu tayari imeweka bajeti ya Sh milioni 35 kwa ajili ya zahanati hiyo.


Amesema kukamilika kwa zahanati hiyo kutafanya Kata ya Mwasubi yenye vijiji vitatu kubakiwa na Kijiji kimoja kisicho na zahanati, huku wananchi wakiendelea na jitihada za kuhakikisha huduma za afya zinaimarika na hatimaye wanapata kituo cha afya katika kata hiyo.


Kupitia mkutano huo Mratibu wa Maafa wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Robert Mhina, ametoa elimu kuhusu maandalizi na tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño na jinsi ya kuchukua hatua za kujikinga, huku Serikali ikisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati yake na wananchi ni muhimu katika kutatua changamoto za maendeleo na kukabiliana na majanga.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi akizungumza na Meneja wa Ruwasa na Tarura wilayani humo kwa njia ya simu kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Mwasubi wa kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili mnamo Oktoba 8, 2026 katika Kijiji cha Ngw’anghili
Diwani wa Kata ya Mwasubi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Samson Gelewa akizungumza kwenye mkuano wa hadhara wa Mkuu wa Wilay ahiyo Mhe. Peter Masindi wenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Kata hiyo uliofanyika katika Kijiji cha Ngw’anghili Oktoba 8, 2026
Mratibu wa Maafa wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Robert Mhina
Kaimu Mshauri wa Jeshi la Akiba wilayani Kishapu mkoani Shinyanga CAPT MS Mhina

Afisa Tarafa ya Mondo wilayani kishapu mkoani Shinyanga Atka Haji

Mtendaji wa Kata ya Mwasubi halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Sigera MsitafaMwenyekiti wa Kijiji cha Ngw’anghili Kata ya Mwasubi wilayani Kishapu mkoani ShinyangaGebu Bunzari Mabere
















































Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com