
Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi imetoa viti na meza 20 vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 3 kwa walimu wa Shule ya Sekondari Mweli iliyopo katika Jimbo la Ushetu, mkoani Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani, ameshiriki katika zoezi la kupokea samani hizo na kueleza kuwa msaada huo utasaidia kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu, kuongeza ufanisi katika ufundishaji na kuchochea ufaulu wa wanafunzi.
Cherehani amesema awali walimu walikabiliwa na changamoto ya upungufu wa viti na meza, hali iliyowalazimu baadhi yao kuchangia samani hizo pamoja na wanafunzi.
“Walimu, kuna wakati mlikuwa mnachangia viti na wanafunzi, lakini sasa tatizo hilo limepatiwa ufumbuzi kupitia Benki ya CRDB. Tunaomba msaada huu uwe kichocheo kikubwa cha kukuza taaluma na kuongeza ufaulu mzuri wa wanafunzi wetu,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana, amesema msaada huo ni sehemu ya mchango wa benki hiyo katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu bora nchini.
Wagana amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mbunge kuhusu upungufu wa meza na viti kwa walimu wa shule hiyo.
“Baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mbunge kuwa shule hii ina upungufu wa meza na viti vya walimu, tuliamua kuwaletea samani hizi kwa lengo la kuinua taaluma. Tunaamini kuwa Serikali pekee haiwezi kukamilisha kila kitu, hivyo ni muhimu wadau wengine kushirikiana katika kuboresha sekta ya elimu,” amesema Wagana.
Ameongeza kuwa Benki ya CRDB ina utaratibu wa kutenga asilimia moja ya faida baada ya kodi kwa ajili ya kurejesha sehemu ya mapato yake kwa jamii na Kupitia kampeni ya Keti jifunze, benki hiyo imekuwa ikichangia upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, ikiwemo madawati na samani nyingine za shule.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mweli amesema awali walimu walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya kuchangia viti na meza na wanafunzi, hali iliyokuwa ikiathiri mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
“Mwanzo tulikuwa tunagombania viti na wanafunzi. Wakati mwingine walimu walikosa kabisa viti, sasa tumepata viti na meza kwa kila mwalimu, hivyo msaada huu utakuwa chachu ya kufanya kazi kwa utulivu na kuleta matokeo chanya katika kuinua taaluma,” amesema Mwalimu Mkuu.
Samani hizo 20 zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 3 zinatarajiwa kusaidia kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu na kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu katika Shule hiyo.








Social Plugin