Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AJALI MBILI MOROGORO WATU 32 WAFARIKI, 37 WAJERUHIWA

Na Lilian Kasenene, Morogoro

WATU 32 wamefariki dunia, wakiwemo askari wa Jeshi la Polisi, huku wengine 37 wakijeruhiwa katika ajali mbili tofauti zilizotokea usiku wa Oktoba 8, mwaka huu, katika maeneo ya Magole wilayani Kilosa na Mkambarani wilayani Morogoro.


Afisa wa Kitengo cha Habari na Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Scholastica Ndunga, alisema Oktoba 8, majira ya saa mbili usiku, hospitali hiyo ilipokea miili ya watu wanne na majeruhi saba waliopata ajali eneo la Dumila, wilayani Kilosa.


Alisema katika ajali ya pili iliyotokea eneo la Mkambarani, wilayani Morogoro, usiku huohuo, hospitali ilipokea miili ya watu 28 na majeruhi 30.


Ndunga alisema kati ya miili iliyotokana na ajali ya Mkambarani, iliyokuwa imetambuliwa kwa kuzingatia jinsia ni ya wanaume 10 na wanawake saba, huku miili 11 ikiwa bado haijatambuliwa kutokana na sehemu kubwa ya miili hiyo kuungua.


Alisema miili hiyo imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.


Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, alithibitisha kutokea kwa ajali hizo mbili na kueleza kuwa ajali ya kwanza ilihusisha askari watatu wa Jeshi la Polisi.


Kantimbo alisema ajali ya kwanza ilitokea eneo la Magole, wilayani Kilosa, na kuhusisha gari la Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro lenye namba za usajili PT 5361 GMW, aina ya pickup, lililokuwa likiendeshwa na askari mwenye namba G9771, SGT Abdallah Ramadhani (37), likitokea Morogoro kuelekea Turiani.


Alisema gari hilo la polisi liligongana na lori lenye namba za usajili T309 EMK, aina ya Scania, lililokuwa na tela lenye namba 424 DUM, likitokea Dodoma kuelekea Dar es Salaam. Dereva wa lori hilo alifahamika kwa jina moja la Amiri.


Aidha, alisema lori hilo liligongana na gari jingine aina ya Scania, lenye namba za usajili T755 AJS na tela lenye namba T897 AJJ, lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Tabora. Gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Juma Mustaph, mkazi wa Tabora.


Amesema chanzo cha ajali hiyo bado kinachunguzwa.


Kuhusu ajali ya pili iliyotokea Mkambarani, Kantimbo alisema ilihusisha basi la abiria aina ya Higer, lenye namba za usajili T672 ELT, mali ya kampuni ya Green Line, lililokuwa likitoka Dar es Salaam kuelekea Mbeya, na lori aina ya Scania, lenye namba za usajili T902 EGN, lililokuwa limebeba shehena ya magogo ya milunda.


Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, lori hilo lilikuwa likiendeshwa na Abdallah (36), mkazi wa Makambako, huku dereva wa basi akitajwa kuwa Silaji Ndosi.


Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Joseph Mwasabeja, alisema kikosi chake kiliongeza magari ya uokoaji baada ya kubaini ukubwa wa ajali na moto uliokuwa umesambaa eneo la tukio.


Mwasabeja alisema hatua ya kwanza ilikuwa kuokoa maisha ya watu, akieleza kuwa kikosi chake kilifanikiwa kutoa miili 29 na kuwasaidia majeruhi 30 kufikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.


Aliongeza kuwa idadi rasmi ya vifo na majeruhi inapaswa kuthibitishwa na wataalamu wa afya.


Miongoni mwa manusura wa ajali hiyo ni Obtato Mwanyigu, ambaye alisema alishuhudia lori likihama upande wake wa barabara na kuelekea upande wa basi walimokuwa wakisafiria.


Majeruhi waliotajwa ni Groli Michael, Issa Said, Sapi Raymond, Buron Waya, Fabian Aduka, Isaya Rachard, Asia Masalanje, Groli Ally, Melata Magolata, Daniel Malagala, Olive Paulo, Carolina Thomasi, Athumani Pazi, Mohamed Abdalla, Jane Petter, Abdikadiri Liwagala, Mohamed Abdikadiri na Omary Abdikadiri.


Majeruhi wengine ni David Paulo, Henry Nyarike, Amani Philipo, Neema Shabani, Consolata Mwalutanile, Shaila Magala, Asina Fundi, Devota Cassian, Rama Salum, Fadhili Kalinga, Anuari Hassan, Opitalu na Londoline.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com