Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

IDARA YA UHAMIAJI YAPONGEZWA KWA KUJENGA MAHUSIANO MAZURI NA WAANDISHI WA HABARI

 

Idara ya Uhamiaji nchini imepongezwa kwa kujenga na kuimarisha mahusiano mazuri na waandishi wa habari, pamoja na kutoa elimu kuhusu majukumu na wajibu wa idara hiyo ili kuwawezesha kuandika habari sahihi na zenye uelewa mpana wa masuala ya uhamiaji.

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Daniel Machunda, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, wakati wa ufunguzi wa kongamano la wadau wa habari lililofanyika Oktoba 12, 2026, katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Chuo cha Benki, jijini Mwanza.

Machunda ameipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kudumisha mahusiano mazuri na wadau wa sekta ya habari, hususan Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA Tanzania).

Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za umma na vyombo vya habari katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na zinazoeleweka kuhusu majukumu ya taasisi hizo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Bw. Edwin Soko, ametoa shukrani za dhati kwa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala, kwa juhudi zake za kuimarisha ushirikiano kati ya Idara ya Uhamiaji na waandishi wa habari nchini.

Soko amesema hatua ya kuwapatia waandishi wa habari elimu kuhusu majukumu ya Idara ya Uhamiaji ni muhimu katika kuongeza uelewa wao na kuwawezesha kutekeleza wajibu wao wa kuhabarisha umma kwa usahihi na weledi.

Katika kongamano hilo, Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji, Bw. Azizi Kirondomara, aliwasilisha mada kuhusu wajibu na majukumu ya Idara ya Uhamiaji nchini, kwa lengo la kuwajengea uwezo wahariri na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu uhamiaji.

Wasilisho hilo lililenga kuwawezesha wadau hao kuelewa vyema majukumu ya idara hiyo, pamoja na kupata maarifa yatakayowasaidia katika kuandaa na kuwasilisha habari zinazohusu masuala ya uhamiaji kwa usahihi zaidi.

Akizungumzia mada hiyo, Bw. Alphonce Tony amesema kuwa wasilisho la Idara ya Uhamiaji limewapa elimu ya kutosha kuhusu masuala mbalimbali ya uhamiaji nchini.

Ameeleza kuwa elimu hiyo itawasaidia wahariri na waandishi wa habari kuboresha uandishi wao, kuongeza usahihi wa taarifa wanazozitoa na kuwasilisha masuala ya uhamiaji kwa uelewa mpana zaidi kwa umma.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na zaidi ya wahariri na waandishi wa habari 60, ambao ni wanachama wa MISA Tanzania, pamoja na wawakilishi kutoka taasisi za serikali, sekta binafsi, viongozi wa dini na taasisi mbalimbali za kihabari.

Kongamano hilo limeendelea kuonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Idara ya Uhamiaji na vyombo vya habari katika kujenga uelewa wa pamoja, kuimarisha mawasiliano na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu majukumu ya Idara ya Uhamiaji nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com