Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HATUJAZUIA BIASHARA HALALI BANDARI YA BAGAMOYO, TUMEZUIA BIASHARA ZA MAGENDO YAKIWEMO MAFUTA YA KULA - TRA

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema haijazuia biashara halali kwenye Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani bali imezuia biashara za magendo yakiwemo mafuta ya kupikia ambayo yamekuwa yakiingizwa nchini bila kufuata utaratibu na kudhoofisha viwanda vya ndani. 

Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Bw. Peter Jackson Eliona kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na mmoja wa wananchi katika mkutano wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba juu ya kuzuiwa kwa biashara Bandari ya Bagamoyo ambapo amesema kuwa TRA haijazuia biashara bali imezuia magendo.

Amesema TRA kupitia Idara ya Forodha inalo jukumu la kuwezesha biashara halali, kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali, kulinda walaji na wafanyabiashara, pamoja na kuhakikisha kuwa mizigo yote inayoingia nchini kutoka nje inafuata taratibu na sheria za nchi.

Ameeleza kuwa kwa msingi huo, TRA haijazuia wafanyabiashara kuingiza mizigo yao kihalali kupitia Bandari ya Bagamoyo na wafanyabiashara wote wanaofuata njia halali wanakaribishwa sana. 

"Tunawakaribisha wafanyabiashara wote wanaotaka kutumia bandari hiyo kwa shughuli zao halali na tunawahakikishia kuwa tupo tayari kuwahudumia kwa kuzingatia taratibu na sheria zilizowekwa,
Hata hivyo, TRA inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kupambana na magendo katika eneo la Bagamoyo, hususan magendo ya mafuta ya kula", amesema Bw. Eliona. 

Amebainisha kuwa hatua hizo zinalenga kulinda mapato ya Serikali, kuhakikisha ushindani wa haki kwa wafanyabiashara wanaofuata sheria, na kuwalinda walaji dhidi ya bidhaa zinazoingia nchini kinyume cha sheria.

"Napenda kutoa msisitizo kwa wote wanaojihusisha na biashara za magendo kuwa TRA itaendelea kutekeleza wajibu wake kwa umakini. Timu zetu zinafanya doria saa 24, zikiwemo doria za baharini kwa kutumia boti na doria za nchi kavu, kwa lengo la kudhibiti magendo na kuhakikisha kuwa biashara zinazofanyika katika eneo hili zinafuata sheria na taratibu husika", amesisitiza Meneja huyo.

Amesema TRA inawakaribisha wafanyabiashara wote wanaotaka kuingiza mizigo yao kwa kufuata sheria, na kuwa  ipo tayari kuwahudumia saa 24 kwa kuzingatia taratibu za Forodha bila usumbufu wowote. 

TRA inaunga mkono biashara halali na tunapinga magendo kwa nguvu zote ili tujenge uchumi imara wa nchi yetu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com