Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC SHINYANGA AMUAPISHA DC MPYA KAHAMA, AWATAKA VIONGOZI KUSIMAMIA MAPATO, KUSIKILIZA WANANCHI


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akizungumza Oktoba 5,2026 wakati wa hafla ya uapisho iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkoa wa Shinyanga. Picha na Kadama Malunde
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akizungumza wakati wa hafla ya uapisho iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkoa wa Shinyanga.

Na Kadama Malunde – Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amewataka Wakuu wa Wilaya kuwa karibu na wananchi, kusikiliza kero zao na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati, huku akiwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha.

Mhe. Mhita ametoa maelekezo hayo leo, Oktoba 5, 2026, wakati akimuapisha Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Dkt. Francis Daudi Mlacha, katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkoa wa Shinyanga, iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mhita amempongeza Dkt. Daudi kwa kuaminiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kumtaka akachape kazi kwa bidii, akishirikiana na viongozi wenzake pamoja na wananchi ili kuharakisha maendeleo ya Kahama.

“Nakupongeza sana kwa kuteuliwa na Rais wetu kuwa Mkuu mpya wa Wilaya ya Kahama, karibu Shinyanga kwenye timu ya ushindi,” amesema Mhe. Mhita.

Katika maagizo yake kwa Wakurugenzi wa Halmashauri sita za Mkoa, amewataka kuongeza mapato ya ndani, kuibua vyanzo vipya na kudhibiti mianya ya upotevu, huku akisisitiza kuwa fedha zinazokusanywa zinapaswa kuelekezwa kwenye huduma na miradi yenye manufaa kwa wananchi.

Amesema Halmashauri zinapaswa kutenga fedha za kukamilisha miradi ya maendeleo iliyoanzishwa, hususan ile iliyoshirikisha nguvu na michango ya wananchi, badala ya kuacha miradi ikiwa haijakamilika.

Mhe. Mhita pia amewataka Wakurugenzi kuhakikisha madeni ya wazabuni yanalipwa na kuchukua tahadhari dhidi ya kuanzisha madeni mapya yasiyo na uhakika wa kulipwa, akisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya fedha za umma.

Katika hatua nyingine, amewataka viongozi kuimarisha usafi wa mazingira, ikiwemo kuzibua mitaro na kuondoa maeneo hatarishi, kama sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Amesema wananchi wanapaswa kupewa elimu ya kutosha kuhusu tahadhari za mvua hizo, huku viongozi wa maeneo mbalimbali wakihakikisha mipango ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza inatekelezwa kwa wakati.

Kwa upande wake, Dkt. Daudi Mlacha, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, akiahidi kutekeleza majukumu yake kwa bidii na kuzingatia maelekezo yaliyotolewa.

Amesema moja ya mambo atakayoanza nayo ni kushughulikia changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara, sambamba na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha fedha zinazopatikana zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya wa Mkoa wa Shinyanga, amemuahidi Dkt. Daudi ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Bwana Mabala Mlolwa, amesema chama hicho kiko tayari kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha changamoto za wananchi zinapatiwa ufumbuzi na utekelezaji wa shughuli za maendeleo unaendelea kwa kasi.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akizungumza wakati wa hafla ya uapisho iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkoa wa Shinyanga.
Mkuu mpya wa wilaya ya Kahama Dk. Francis Daudi Mlacha akipishwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita.
Mkuu mpya wa wilaya ya Kahama Dk. Francis Daudi Mlacha akipishwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita.
Mkuu mpya wa wilaya ya Kahama Dkt. Francis Daudi Mlacha akipishwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akizungumza wakati wa hafla ya uapisho iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkoa wa Shinyanga.



















Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com