
Na Mwandishi wetu - Malunde Blog
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amewataka waendesha bodaboda katika Kanda ya Maganzo, Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, kuzingatia sheria, kudumisha amani na kutanguliza usalama katika shughuli zao za kila siku.
Kamanda Magomi ametoa rai hiyo Oktoba 7, 2026, wakati wa utekelezaji wa programu ya “Ongea na Kamanda wa Mkoa wa Shinyanga”, iliyofanyika katika Uwanja wa Sabasaba, Kijiji na Kata ya Maganzo, ambapo alikutana na waendesha bodaboda pamoja na kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya usalama.
Akiwa ameambatana na maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali, SACP Magomi aliwataka waendesha bodaboda kuhakikisha usalama wao unakuwa kipaumbele wakati wote wanapotekeleza majukumu yao, ikiwemo kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.
Alisisitiza umuhimu wa utii wa sheria bila shuruti, akiwataka wananchi kufuata sheria za nchi kwa hiari na kutambua kuwa utekelezaji wa sheria ni sehemu muhimu ya kujenga jamii yenye amani, utulivu na maendeleo.
Kamanda Magomi pia alieleza kuwa amani na usalama ni msingi wa shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya wananchi, hivyo waendesha bodaboda wanapaswa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na mamlaka nyingine katika kuhakikisha amani na usalama vinadumishwa katika maeneo yao.
Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño zinazotarajiwa katika msimu huu, ikiwemo kuhakikisha mazingira yanakuwa salama kwa kusafisha mitaro na maeneo mengine yanayoweza kusababisha maji kutuama au kujaa.
Aidha, Kamanda Magomi alitoa elimu kuhusu kampeni ya usalimishaji wa hiari wa silaha haramu, akiwataka wananchi wenye silaha hizo kuzisalimisha kwa hiari kabla ya kufikia mwisho wa kampeni hiyo tarehe 31 Oktoba 2026.
Vilevile, aliwakumbusha wananchi kutojichukulia sheria mkononi na badala yake kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pale wanapokutana na changamoto zinazohitaji hatua za kisheria.
Kamanda Magomi achangia Sh100,000 kwa waendesha bodaboda
Katika tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, alichangia kiasi cha Shilingi 100,000 katika mfuko wa wanachama wa waendesha bodaboda Kanda ya Maganzo.
Mchango huo umetolewa kwa lengo la kuhamasisha waendesha bodaboda kuwa na umoja na mfuko wa kusaidiana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kijamii zinazoweza kujitokeza miongoni mwao.
Kamanda Magomi amewataka waendesha bodaboda kuendelea kushirikiana na kujenga utamaduni wa kusaidiana, huku wakizingatia sheria na kanuni zinazosimamia shughuli zao.
Waendesha bodaboda waomba msaada wa kupata leseni
Kwa upande wao, waendesha bodaboda walimpongeza Kamanda Magomi kwa kufika Maganzo na kutoa elimu kuhusu usalama, sheria na umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi.
Walisema elimu hiyo imewasaidia kufahamu kwa kina wajibu wao katika kulinda usalama wao, abiria na watumiaji wengine wa barabara, huku wakiahidi kuzingatia maelekezo yaliyotolewa.
Aidha, waliwasilisha changamoto ya baadhi yao kushindwa kupata leseni za kuendesha vyombo vya moto, licha ya kusoma mafunzo na kupata vyeti kutoka katika vyuo walivyosomea.
Kwa mujibu wa waendesha bodaboda hao, changamoto hiyo inatokana na baadhi ya vyuo walivyosomea kutotambulika au kutoonekana katika mfumo unaotumika katika mchakato wa kupata leseni.
Akijibu changamoto hiyo, Kamanda Magomi aliwaahidi kuwasaidia kwa kuwaunganisha na wakufunzi kutoka katika vyuo vilivyosajiliwa, ili waweze kupata mafunzo kwa gharama nafuu na hatimaye kukidhi masharti ya kupata leseni za kuendesha vyombo vya moto.
Waendesha bodaboda hao pia walilipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendelea kushirikiana nao na kuwataka kuendeleza ushirikiano huo kwa ajili ya kuimarisha usalama, amani na shughuli za kiuchumi katika eneo la Maganzo.






Social Plugin