Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIKUNDI 42 VYATAKIWA KUREJESHA FEDHA ZA MIKOPO

Diwani wa kata ya mjini jimbo la Songea mjini Mathew Ngalimanayo akizungumza katika taarifa ya  utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2025/2030 kwa kipindi cha mwaka 2025/2026

Na Regina Ndumbaro, Songea-Ruvuma

Vikundi 42 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu vilivyonufaika na mikopo katika Kata ya Mjini, Manispaa ya Songea, vimetakiwa kurejesha fedha walizokopa ili kuwawezesha wananchi wengine kunufaika na fursa hiyo. 

Akisisitiza umuhimu wa urejeshaji wa mikopo hiyo, Mwenyekiti wa Kata ya Mjini, Lothal Nikata, amesema baadhi ya akina mama na vijana waliopata mikopo ya pikipiki wamejikuta wakinyang’anywa pikipiki hizo kutokana na kutorejesha fedha kwa wakati, huku akiwataka wanufaika kutimiza wajibu wao na kuhakikisha mikopo hiyo inarejeshwa.

Nikata pia amewataka wenyeviti wa mitaa katika kata hiyo kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kusoma taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi pamoja na kusimamia kwa karibu shughuli za maendeleo katika maeneo yao. 

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mjini, Mathew Ngalimanayo, akisoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025/2030 kwa kipindi cha mwaka 2025/2026, amesema jumla ya vikundi 103 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu vimesajiliwa, huku vikundi saba vikifanikiwa kupata fedha taslimu kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kiuchumi na ujasiriamali.

Katika sekta ya elimu, Ngalimanayo amesema madarasa matatu yamejengwa katika Shule ya Msingi Majimaji kwa gharama ya Sh milioni 96, huku uchimbaji wa kisima katika shule ya msingi Mfaranyaki ukikamilika. 

Amesema pia jamii imeanza kupewa elimu kuhusu mpango wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto unaolenga maeneo matano ambayo ni lishe, afya, ujifunzaji wa awali, malezi yenye mwitikio pamoja na nidhamu. 

Kwa upande wa sekondari, amesema uzio umejengwa katika shule ya wasichana Songea kwa kutumia Sh milioni 20.5 kutoka mapato ya ndani ya Manispaa ya Songea, huku fedha zikipokelewa kwa ajili ya ujenzi wa matundu matatu ya vyoo kwa wanafunzi wenye ulemavu. 

Aidha, amesema wanaendelea kuboresha ufaulu na nidhamu pamoja na kupokea ruzuku za Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa elimu bila ada katika shule za msingi na sekondari.

Katika eneo la miundombinu, Ngalimanayo amesema kata hiyo imefanikiwa kuboresha baadhi ya barabara kwa kiwango cha lami, kuweka taa za barabarani na kuanza ujenzi wa mitaro, akitaja barabara ya CCM/Mahenge. 

Amesema barabara ya SOUWASA/Mashujaa imepangwa kujengwa kwa kiwango cha lami katika mwaka wa fedha 2026/2027. 

Aidha, amesema wanaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha jengo la utawala katika Shule ya sekondari Mashujaa, kuboresha mazingira ya eneo la Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata pamoja na ununuzi wa samani. 

Hata hivyo, wananchi wamewasilisha changamoto zikiwemo ujenzi wa vivuko, ukamilishaji wa jengo la mabweni, ujenzi wa mitaro katika barabara ya SOUWASA/Mashujaa na mtaro imara katika eneo la Makumbusho/Mahenge.

Kata ya Mjini yenye mitaa minne ina jumla ya wakazi 7,419 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, wakiwemo wanawake 3,648 na wanaume 3,771, ikiwa na jumla ya kaya 2,127. 

Akitoa taarifa hiyo leo Septemba 28, 2026 katika Ukumbi wa Kata ya Mjini, Ngalimanayo amesema kata hiyo pia inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari zinazohusiana na El Niño, ikiwemo kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji na kingo za mito, kutupa taka kwenye mitaro na maeneo ya mapito ya maji, kuchimba mchanga mabondeni na kutiririsha maji taka ovyo. 

Amesema wananchi wanaendelea kuhamasishwa kujenga nyumba imara, kuweka mazingira katika hali ya usafi, kujiandaa dhidi ya magonjwa ya mlipuko, kuweka akiba ya chakula na kutumia fedha kwa matumizi yenye tija, huku akieleza kuwa changamoto zilizowasilishwa na wananchi ziko katika mchakato wa kutatuliwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com