Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TEA YATENGA SH1.3 BILIONI KUJENGA HOSTELI IPA PEMBA


Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imetenga takribani Sh1.3 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa hosteli katika Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA) Kampasi ya Pujini Pemba, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia chuoni hapo.

Fedha hizo zitatumika kutekeleza mradi huo baada ya TEA na IPA kusaini mkataba maalumu wa ushirikiano wa ujenzi wa hosteli hiyo, katika hafla iliyofanyika Septemba 8, 2026.

Mkurugenzi Mkuu wa TEA Dkt. Erasmus Kipesha alisema, uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za mamlaka hiyo kufadhili miradi ya elimu yenye lengo la kuongeza ubora na upatikanaji wa elimu nchini.

Alisema, TEA kama taasisi ya Muungano ina wajibu wa kushiriki katika kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji, huku akiitaka IPA kuhakikisha mradi huo unaanza na kukamilika kwa wakati.

“Ni imani yangu kuwa mradi huu ukikamilika utaongeza ufanisi katika ujifunzaji na ufundishaji, lakini pia kuongeza uwezo wa chuo kutoa huduma kwa wananchi na kuimarisha huduma za mafunzo kwa maendeleo ya sekta ya elimu,” alisema Dkt. Kipesha.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa IPA Dkt. Hamad Khamis Said alisema, kukamilika kwa hosteli hiyo kutasaidia kupunguza changamoto ya malazi kwa wanafunzi na kuwawezesha kutumia muda mwingi katika masomo.

Alisisitiza kuwa, mradi huo utakuwa na matokeo chanya katika maendeleo ya taaluma chuoni, pamoja na kuboresha mazingira ya watumishi wa umma wanaopata mafunzo katika taasisi hiyo.

Dkt. Said alisema, TEA imekuwa mdau muhimu katika kuboresha miundombinu ya chuo, akitaja ruzuku iliyotolewa na mamlaka hiyo katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya ukarabati wa maabara ya kompyuta pamoja na ununuzi wa kompyuta.

“Ujenzi wa bweni hili kwetu sisi ni wa thamani sana na utaacha kumbukumbu kwa vizazi vijavyo hata kama hatutakuwepo. Tunawashukuru sana TEA kwa kuendelea kuwa sehemu ya uboreshaji na maendeleo ya chuo chetu,” alisema Dkt. Said.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa Kampasi ya Pujini kutoa huduma bora za malazi na kwa ujumla kuchangia uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia na utoaji wa mafunzo katika Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com