Tanzania imejipanga kikamilifu kuvutia mitaji na teknolojia kutoka kwa wawekezaji wa Marekani, hususan katika sekta ya afya na uzalishaji wa dawa, huku ikilenga kujenga ushirikiano wa muda mrefu utakaowanufaisha Watanzania na vizazi vijavyo.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, wakati akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Ushirikiano wa Afya uliofanyika Washington, D.C., nchini Marekani.
Waziri Mchengerwa alisema Tanzania inahitaji kuendeleza ushirikiano wa kimkakati na wawekezaji wa Marekani, akitolea mfano ushirikiano wa kihistoria uliofanyika katika miaka ya 1970 kupitia kampuni ya McKinsey & Company, ambao ulisaidia kujenga taasisi imara ambazo zinaendelea kutoa mchango nchini hadi leo.
Alisisitiza kuwa Tanzania kwa sasa inalenga zaidi ya miamala ya kawaida ya kibiashara, bali inataka kujenga ushirikiano wa kudumu wa uwekezaji, teknolojia na utaalamu ambao utakuwa na manufaa kwa pande zote na kuleta matokeo yatakayodumu kwa vizazi vijavyo.
Katika hatua hiyo, Chama cha Wafanyabiashara cha Marekani kimeahidi kushirikiana na Tanzania katika kuleta wawekezaji kutoka sekta ya dawa nchini humo ili kuangalia fursa za uwekezaji katika uzalishaji wa dawa na bidhaa za afya nchini Tanzania.
TANZANIA YAIMARISHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI
Waziri Mchengerwa alisema chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na falsafa ya 4R, Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini pamoja na miundombinu muhimu inayohitajika na wawekezaji.
Alisema uwekezaji katika miundombinu, ikiwemo upatikanaji wa nishati ya uhakika kupitia Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), unaongeza uwezo wa Tanzania kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya nchini kote, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya uzinduzi wa Bima ya Afya kwa Vifaa na Huduma kwa Wote, inayolenga kuhakikisha Watanzania zaidi ya milioni 60 wanapata huduma za afya kwa ufanisi.
LENGO NI TANZANIA KUZALISHA DAWA BADALA YA KUAGIZA
Katika mkakati wa kubadilisha Tanzania kutoka kuwa nchi inayotegemea uagizaji wa dawa kutoka nje kwenda kuwa nchi inayozalisha dawa kwa kiwango kikubwa, Wizara ya Afya imechukua hatua mbalimbali za kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji.
Miongoni mwa hatua hizo ni kuundwa kwa Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji katika Sekta ya Dawa (PIAT) pamoja na kutengwa kwa eneo maalum la kiuchumi huko Mloganzila, litakalotumika katika kukuza uwekezaji katika sekta ya dawa.
Pia, Serikali ina mpango wa kuanzisha Kiwanda cha Taifa cha Uzalishaji wa Chanjo na Bidhaa za Kibiolojia, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa Tanzania kuzalisha bidhaa muhimu za afya ndani ya nchi.
Sambamba na hilo, Tanzania inaendelea kutoa unafuu wa kodi kwa baadhi ya malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa dawa, kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani.
TMDA YAFIKIA KIWANGO CHA 3 CHA WHO
Waziri Mchengerwa pia alieleza kuwa juhudi za kuvutia uwekezaji katika sekta ya dawa zinaungwa mkono na mafanikio ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) kufikia Kiwango cha 3 cha Shirika la Afya Duniani (WHO) katika mifumo ya udhibiti wa dawa.
Hatua hiyo imeongeza uaminifu wa mifumo ya udhibiti wa dawa nchini na kurahisisha Tanzania kuendana na viwango vya kimataifa, ikiwemo mifumo ya udhibiti inayotumika katika masoko makubwa kama Marekani.
TANZANIA KITUO CHA SOKO LA ZAIDI YA WATU MILIONI 300
Aidha, uteuzi wa Tanzania kuwa mwenyeji wa Huduma za Ununuzi wa Pamoja za SADC umefungua fursa kubwa zaidi kwa wawekezaji katika sekta ya dawa na bidhaa za afya.
Kupitia nafasi hiyo, Tanzania inaweza kuwa kituo muhimu cha uzalishaji na usambazaji wa dawa kwa soko la kikanda la SADC lenye zaidi ya watu milioni 300 katika nchi 16 wanachama.
Kwa hatua hiyo, Serikali inaona fursa hiyo kuwa kichocheo muhimu cha uwekezaji katika viwanda vya dawa, chanjo na bidhaa nyingine za afya, huku Tanzania ikijiimarisha kama kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za afya katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Social Plugin