TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Kongamano la Sita la Jumuiya ya Taasisi za Mitaala Afrika (ACA), litakalofanyika Septemba 22 hadi 25, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, alisema kongamano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano na Taasisi ya Elimu Zanzibar (TEZ), pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.
Dkt. Komba alisema Tanzania ilipewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa kongamano hilo wakati wa kongamano la tano lililofanyika Abuja, Nigeria, mwaka 2025, na maandalizi yake yameendelea kufanywa kwa ushirikiano na Jumuiya ya Taasisi za Mitaala Afrika.
Alisema kaulimbiu ya kongamano hilo inalenga mageuzi ya mifumo ya elimu barani Afrika, maboresho ya mitaala, maandalizi ya walimu pamoja na ubunifu jumuishi katika matumizi ya Akili Unde na teknolojia zinazoibuka.
Kwa mujibu wa Dkt. Komba, kongamano hilo litawakutanisha wataalamu wa mitaala, watafiti, watunga sera, walimu, wakufunzi, wahadhiri, wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu pamoja na wadau wengine kutoka Afrika na sehemu mbalimbali duniani.
Alisema Tanzania itatumia fursa hiyo kuonesha mafanikio katika sekta ya elimu, ikiwemo maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la mwaka 2023, mifumo ya elimu na mitaala, huku pia ikibadilishana uzoefu na nchi nyingine za Afrika.
Kongamano hilo linatarajiwa kujumuisha uwasilishaji wa makala 80, majadiliano, maonyesho ya bunifu na teknolojia za kielimu pamoja na ziara ya kielimu. Miongoni mwa matokeo yanayotarajiwa ni Azimio la Dar es Salaam kuhusu Mageuzi ya Elimu Barani Afrika na mapendekezo ya matumizi ya Akili Unde katika mitaala.
Dkt. Komba alisema mgeni rasmi katika ufunguzi wa kongamano hilo anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratias John Ndejembi, huku akiwataka wadau wa elimu na wanahabari kushiriki kikamilifu katika kufanikisha kongamano hilo.













Social Plugin