Na Dotto Kwilasa,Dodoma
SERIKALI imewataka wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kuhakikisha uchaguzi wa viongozi wapya unafanyika kwa amani, utulivu na kuzingatia Katiba, huku viongozi watakaopatikana wakisisitizwa kuutazama uongozi kama dhamana ya kuwatumikia wanachama.
Wito huo umetolewa leo, Septemba 17, 2026, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa TALGWU jijini Dodoma.
Sangu amesema nafasi ya uongozi katika chama cha wafanyakazi si fursa ya kutawala, bali ni dhamana inayowataka viongozi kusikiliza, kuelewa na kushughulikia changamoto zinazowakabili wanachama.
“Uongozi ni utumishi, si kutawala,” amesema Sangu.
Amesema viongozi watakaopata dhamana hiyo wanapaswa kuwa tayari kusikiliza kero za wanachama na kuzishughulikia kwa uadilifu, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda umoja na mshikamano wa chama.
Akirejea maandiko ya Biblia katika Marko 10:45 na Mathayo 20:26-27, Waziri huyo amesema viongozi wanapaswa kutambua kuwa msingi wa uongozi ni kuwahudumia wengine.
Amesema uchaguzi huo haupaswi kuwa chanzo cha migawanyiko miongoni mwa wanachama, bali utumike kama fursa ya kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya TALGWU.
Sangu pia amewapongeza viongozi na wanachama wa TALGWU kwa kudumisha amani, utulivu na ushirikiano ndani ya chama, akisema hali hiyo ni muhimu katika kujenga mahusiano mazuri kati ya Serikali na wafanyakazi.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali inatambua na kuthamini haki pamoja na maslahi ya wafanyakazi, huku akieleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kushirikiana na vyama vya wafanyakazi kupitia mfumo wa majadiliano kati ya pande hizo (Social Dialogue).
Kwa mujibu wa Sangu, mfumo huo ni muhimu katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili watumishi, ikiwemo stahiki za uhamisho, malimbikizo ya madeni na masuala mengine yanayohusu maslahi ya wafanyakazi.
Kauli hiyo imekuja wakati TALGWU ikiwasilisha mbele ya mkutano huo changamoto zinazowakabili watumishi wa Serikali za Mitaa na kuiomba Serikali kuendelea kuzitafutia ufumbuzi.
Akizungumza katika mkutano huo, Kaimu Katibu Mkuu wa TALGWU, Wandiba Ngocho, amesema chama hicho kimeainisha changamoto sita zinazohitaji hatua zaidi za Serikali kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi, maslahi ya wafanyakazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amezitaja changamoto hizo kuwa ni ucheleweshaji wa fedha za likizo, ucheleweshaji wa malipo ya posho na leseni za huduma kwa baadhi ya watumishi wa kada za afya, stahiki za uhamisho, utekelezaji wa mfumo wa PEPMIS, miundo ya utumishi na mchakato wa kubadilishiwa kada (re-categorization), pamoja na kutofanya kazi kwa ufanisi kwa baadhi ya Mabaraza ya Wafanyakazi.
Ngocho amesema baadhi ya watumishi hupokea stahiki za likizo kwa awamu au baada ya muda uliopangwa, hali ambayo amesema inahitaji kufanyiwa kazi ili kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Amesema pia watumishi wanaohamishwa kutoka kituo kimoja cha kazi kwenda kingine hukumbana na ucheleweshaji wa malipo ya stahiki za uhamisho.
Kuhusu PEPMIS, Ngocho amesema bado kuna changamoto katika utekelezaji na matumizi ya mfumo huo, hivyo ameiomba Serikali kuendelea kufanya maboresho yatakayorahisisha matumizi yake kwa watumishi.
Amesema baadhi ya watumishi pia hukutana na vikwazo katika mchakato wa kubadilishiwa kada kulingana na elimu na ujuzi walioupata, akisisitiza umuhimu wa suala hilo kuangaliwa ili kuwawezesha kutumia taaluma zao ipasavyo katika utumishi wa umma.
Aidha, TALGWU imeomba kuimarishwa kwa utendaji wa Mabaraza ya Wafanyakazi katika halmashauri na taasisi, ili yaweze kutekeleza ipasavyo jukumu la kuwashirikisha wafanyakazi katika masuala yanayohusu ajira na mazingira ya kazi.
Ngocho amezipongeza jitihada za Serikali katika kusikiliza na kushughulikia changamoto za wafanyakazi, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha zaidi majadiliano kati ya Serikali na wafanyakazi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TALGWU, Tumaini Nyamhokya, amesema ushirikiano uliopo kati ya chama hicho na Serikali umeendelea kuwa muhimu katika kushughulikia masuala ya wafanyakazi.
Nyamhokya amesema mawasiliano ya karibu na viongozi wa Serikali yamesaidia kupunguza migogoro na kuongeza tija kwa watumishi.
Amesema vikao mbalimbali vya chama, ikiwemo Kamati ya Utendaji na Baraza Kuu, vimefanyika kwa amani na utulivu, hali ambayo amesema imeweka mazingira mazuri kuelekea uchaguzi wa viongozi wapya.
Ameeleza kuwa TALGWU itaendelea kushirikiana ndani ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania katika kulinda haki na maslahi ya watumishi nchini.
Mkutano huo umehudhuriwa pia na viongozi na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi kutoka Kenya, Somalia na Malawi, pamoja na viongozi wastaafu wa TALGWU, akiwemo Katibu Mkuu Mstaafu, Rashid Mtega.
Akihitimisha hotuba yake, Sangu amewataka wajumbe watakaopata dhamana ya kuongoza TALGWU na wale ambao hawatachaguliwa kuendelea kushirikiana baada ya uchaguzi, akisisitiza kuwa tofauti za uchaguzi hazipaswi kuvuruga umoja wa chama.
Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kujenga chama chenye nguvu na mshikamano, kitakachoweza kusimamia kwa ufanisi maslahi ya watumishi wa Serikali za Mitaa.

Social Plugin