📌Lengo ni kuwapa fursa zaidi kuwakuza kitaaluma;
📌Ahimiza elimu ya biashara kuwekewa mkazo mashuleni na kuwapongeza shule ya Canossa kwa kazi nzuri inayofanya.
Na Mwandishi wetu
Imeelezwa kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisheria na kisera kuhakikisha mtoto wa kike analindwa dhidi ya mimba za umri mdogo, ndoa za mapema na ubaguzi wa aina yoyote, huku wasichana wakihimizwa kujiendeleza kitaaluma na kushiriki kikamilifu katika fursa za uongozi shuleni, vyuoni na katika jamii.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, Septemba 19, 2026, katika mahafali ya 18 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Canossa, jijini Dar es Salaam, akieleza kuwa wahitimu hao ni miongoni mwa watekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema katika miaka 25 ijayo, idadi ya watu nchini inatarajiwa kuongezeka kutoka milioni 70, hivyo maarifa waliyoyapata yatawasaidia kujiandaa na maisha na mahitaji ya jamii ya wakati huo.
Mhe. Londo amesema kila msichana anayepata elimu ana fursa ya kuwa daktari, wakili, mwalimu na mtaalamu wa kada nyingine. Ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka mkazo katika elimu ya mtoto wa kike, hususan sayansi, huku uwekezaji katika elimu, afya na teknolojia ukiwa sehemu ya kuwaandaa wasichana kukabiliana na changamoto na kuchangia maendeleo ya taifa.
Amesisitiza kuwa maarifa na ujuzi wanaoupata wanafunzi shuleni ni msingi wa kujenga taifa imara na kujiandaa kukidhi mahitaji ya baadaye ya huduma za afya na sekta nyingine. Hivyo, uwekezaji katika elimu na kuwawezesha wasichana kushiriki katika sayansi, teknolojia na uongozi ni muhimu katika kutatua changamoto za jamii na kuendeleza Taifa.




Social Plugin