Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA
Maafisa usafi Manispaa ya Shinyanga, wameiomba Manispaa hiyo kuwalipa malimbizo ya madai yao, wakisema hatua hiyo itawawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi na kuhakikisha mji huo unaendelea kuwa katika hali ya usafi.
Wamebainisha hayo Septemba 19,2026 kupitia risala yao iliyosomwa na Afisa Usafi, Amos Paul, katika kikao cha maafisa usafi wa Manispaa ya Shinyanga.
Paul amesema, pamoja na malimbizo ya madeni yao, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kukusanyia na kuzoa taka, hali inayofanya kazi yao kuwa ngumu.
Aidha, amesema changamoto nyingine wanayokabiliana nayo ni mfumo wa TAUSI pamoja na hitilafu za mifumo ya benki, ambazo zimeathiri ukusanyaji na uwasilishaji wa mapato, hasa katika kipindi cha mwezi Agosti na Septemba.
“Changamoto za mifumo zimekuwa zikikwamisha ukusanyaji wa mapato,” amesema Paul.
WADAU WAOMBA VIFAA VYA USALAMA
Mkurugenzi wa ATA Safari and Lodges na mdau wa usafi, Alfred Mlahi, amewaomba wadau wa mazingira na usafi kushirikiana katika kuwapatia vifaa vya usalama, ikiwemo “Reflector” kwa wafanya usafi, hasa wanaofanya kazi za kufagia barabarani.
Amesema vifaa hivyo vitasaidia kuongeza usalama wao wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Pia amewataka wananchi kupewa elimu kuhusu ulipaji wa ushuru, ili waweze kulipa kwa wakati na kwa hiari, hatua ambayo itasaidia maafisa usafi kupata stahiki zao kwa wakati na kuongeza mapato ya Manispaa.
MSTAHIKI MEYA ATOA AHADI
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mgeni Rasmi katika kikao hicho, ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Salumu Kitumbo, amesema atahakikisha maafisa usafi wenye malimbizo ya madai wanalipwa kwa wakati.
Amesema, pamoja na malipo hayo, ataendelea kushirikiana na wahusika kuhakikisha maafisa hao wanapata stahiki zao kwa wakati, ili waweze kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
MTAA WA MITI MIREFU WATAJWA KWA USAFI
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Miti Mirefu, Nasoro Walioba, amesema mtaa huo umeshika nafasi ya tatu kwa usafi nchini Tanzania, kutokana na juhudi zinazofanywa na maafisa usafi wa Manispaa hiyo.
Amesema mafanikio hayo yanaonesha umuhimu wa kuendelea kuwaunga mkono wafanyakazi wanaohusika na usafi wa mazingira.
Katika kuunga mkono juhudi za kukabiliana na changamoto za usafi, mdau wa mazingira, Salum Abeid, amechangia vifaa vya usafi vikiwemo “Reflector” 50, na kuahidi kutoa toroli mbili za kuzoa taka.
Amesema msaada huo unalenga kuongeza uwezo wa maafisa usafi katika ukusanyaji wa taka na kuboresha mazingira ya Manispaa ya Shinyanga.
MAAFISA USAFI WAOMBA KUTHAMINIWA
Naye Mwakilishi wa Networking Youth Group, Vitalis Bernard Alley, amesema siku hiyo wamejiona kuwa wamepewa thamani baada ya kuona kuwa hawajapewa thamani kutokana na kazi ngumu wanayoifanya kwa zaidi ya miaka kadhaa.
Amesema wamekuwa wakifanya kazi hiyo kwa bidii ili kuhakikisha wanapata mahitaji yao ya msingi, ikiwamo chakula, huku akimuomba Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga kuwa mlezi wao na kuwawakilisha katika changamoto wanazokabiliana nazo.
Amesema malipo yao yanapitia Halmashauri, hivyo amemuomba Mstahiki Meya awapiganie ili watambuliwe na kuthaminiwa na wadau, pamoja na kusaidiwa kupata vifaa vya kisasa vitakavyowawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Aidha, amewaomba viongozi kuhakikisha akina baba na mama wanaofanya kazi kwenye mitaro wanawahi kulipwa stahiki zao, kwa kuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu na yenye changamoto.
TAZAMA PICHA👇👇
Mwenyekiti wa Mtaa wa Miti Mirefu Nassoro Warioba akizungumza.
Social Plugin