Na Dotto Kwilasa,Dodoma
DODOMA. Safari ya takribani miaka nane ya ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma imefikia kilele, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitarajiwa kuuzindua rasmi Septemba 8, 2026. Uzinduzi huo utahusisha majengo ya Wizara 26, taasisi 11 za Serikali pamoja na mtandao wa barabara za lami wenye urefu wa kilomita 57.1.
Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 6, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema kukamilika kwa Mji wa Serikali ni hatua muhimu katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu yenye miundombinu ya kisasa na mazingira bora ya utendaji. Amesema uzinduzi utafanyika katika Uwanja wa Mashujaa uliopo ndani ya Mji huo.
Profesa Kabudi amesema safari ya Mtumba ilianza mwaka 2018, ambapo Novemba 28, 2018 Serikali ilianza kujenga majengo 23 ya muda kwa ajili ya ofisi za Serikali. Majengo hayo yalikamilika Machi 22, 2019 na kuwezesha baadhi ya Wizara na taasisi kuanza kufanya kazi eneo hilo, wakati maandalizi ya ujenzi wa majengo ya kudumu yakiendelea.
Amesema awamu ya pili ya ujenzi ilianza Oktoba 2021, ikilenga kujenga majengo ya kudumu pamoja na miundombinu ya kisasa. Awamu hiyo imehusisha ujenzi wa barabara za lami zenye kilomita 57.1, miundombinu ya maji safi na maji taka, umeme wa chini ya ardhi wenye urefu wa kilomita 42, mawasiliano, TEHAMA, CCTV, kituo cha zimamoto na uboreshaji wa mandhari.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, majengo hayo mapya yameandaliwa kutoa mazingira ya kisasa ya kazi kwa jumla ya watumishi 18,510. Usanifu wake umezingatia ukubwa na mahitaji ya taasisi mbalimbali, huku majengo yakipangwa katika mifumo yenye uwezo wa kuhudumia watumishi kuanzia 150 hadi 1,400 kwa jengo,kulingana na mahitaji ya taasisi husika.
Ujenzi wa awamu ya pili pia umehusisha kwa kiasi kikubwa wataalamu na taasisi za ndani. Jumla ya wakandarasi 11 walishiriki, wakiwamo taasisi tano za Serikali na kampuni sita za sekta binafsi, huku washauri elekezi wote watano wakiwa taasisi za Serikali. Miongoni mwa taasisi hizo ni TBA, NHC, ABECC, MUST na Watumishi Housing Investment.
Profesa Kabudi amesema Mtumba haukujengwa kama mkusanyiko wa majengo ya ofisi pekee, bali umeandaliwa kwa dhana ya ‘smart city’ na mji wa kijani. Miundombinu hiyo imezingatia matumizi ya teknolojia, nishati mbadala, uvunaji wa maji ya mvua, utunzaji wa mazingira, mifumo ya usalama na matumizi bora ya rasilimali ili kuufanya mji huo uwe endelevu kwa miaka ijayo.
Katika utekelezaji wa mradi huo, taasisi mbalimbali za Serikali zimehusika kulingana na majukumu yao. TARURA imehusika na barabara, DUWASA maji safi na maji taka, TANESCO umeme, TTCL mawasiliano, TEMESA mifumo ya CCTV, e-GA TEHAMA, TPDC gesi asilia, Jeshi la Zimamoto huduma za uokoaji na TFS upandaji miti pamoja na uboreshaji wa mandhari.
Mbali na miundombinu, Serikali imekamilisha pia ununuzi na ufungaji wa samani katika ofisi za Wizara 26 na taasisi zitakazotumia majengo hayo, ili kuhakikisha zinaanza kutumika zikiwa tayari kwa shughuli. Mtandao wa barabara za lami wa kilomita 57.1 nao utaunganisha maeneo mbalimbali ya Mji wa Serikali na kurahisisha usafiri kwa watumishi, wananchi na wageni.
Kwa Dodoma, Profesa Kabudi amesema maendeleo ya Mtumba yana maana zaidi ya ujenzi wa majengo ya Serikali, kwa kuwa eneo hilo limekuwa alama ya utekelezaji wa uamuzi wa kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Serikali. Uzinduzi wa Septemba 8 utakuwa kilele cha safari iliyoanza mwaka 2018 na sasa kuufanya Mtumba kuwa sura ya Dodoma mpya ya Serikali, ikibeba historia ya uwekezaji wa taifa, teknolojia, miundombinu ya kisasa na mazingira endelevu.







Social Plugin