Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC MHITA AAGIZA USAFI KILA JUMAMOSI SHINYANGA, ATOA TAHADHARI YA MVUA ZA EL NIÑO

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita

Na Stela Paul , Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kutekeleza zoezi la usafi wa mazingira kila Jumamosi, akieleza kuwa usafi si jukumu la siku moja bali ni sehemu ya nidhamu na maisha ya kila siku.

Mhe. Mhita ameyasema hayo leo, Septemba 25, 2026, wakati akiongoza viongozi mbalimbali wa mkoa na wilaya pamoja na wananchi katika zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika katika Soko la Ujasiriamali la Ibinzamata, mjini Shinyanga.

Zoezi hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa kampeni ya usafi wa mazingira inayolenga kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika kutunza mazingira na kuyafanya kuwa safi na salama.

Akizungumza baada ya zoezi hilo, Mhe. Mhita amesema siku ya Jumamosi imeelekezwa kuwa siku maalumu ya usafi wa mazingira kuanzia ngazi ya kaya, huku akiwataka viongozi wa serikali za mitaa na vijiji kuweka utaratibu utakaowezesha zoezi hilo kutekelezwa kwa ufanisi.

“Kila Jumamosi kazi ya kwanza ni kuhakikisha unaangalia usafi wa eneo lako. Haimaanishi kwamba siku nyingine usafi usizingatiwe. Usafi ni jukumu la kila siku na usafi ni nidhamu,” amesema Mhe. Mhita.

Ameagiza pia Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani Shinyanga kuhakikisha wanawasilisha tathmini za kila mwezi kuhusu mwenendo wa usafi katika kata na maeneo mbalimbali, ili kubaini changamoto na kuchukua hatua stahiki.

“Wakurugenzi wote wanatakiwa kuleta tathmini ya kila mwezi ya taarifa ya mwenendo wa usafi kwa kata na maeneo yote, maana ni lazima tuchukue hatua kwenye maeneo yote machafu, ikiwemo kuchukua hatua za kisheria na kutoza faini pale inapobidi. Usalama wetu sote ni kuzingatia usafi,” ameongeza.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mhita amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi, ikiwemo mabondeni na maeneo yanayoweza kuathiriwa na mvua, kuchukua tahadhari mapema ili kujikinga dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua.

Amesema wananchi wanapaswa kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mamlaka husika, ikiwa ni pamoja na kuondoka katika maeneo hatarishi endapo wataelekezwa kufanya hivyo.

“Kwa wenzetu wote ambao mnakaa kwenye mabonde, majarubuni na maeneo yote hatarishi, tunawasihi kuchukua hatua mapema. Tunatarajia kuwa na mvua za El Niño, hivyo kuchukua tahadhari mapema ni muhimu ili kuhakikisha uhai haupotei, madhara hayajitokezi kwenye miundombinu na wananchi kwa ujumla,” amesisitiza.

Mhe. Mhita amesema Serikali imeendelea kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua, ikiwemo changamoto za kiafya na magonjwa ya mlipuko, akisisitiza kuwa afya na usalama wa wananchi ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, amesema suala la usafi wa mazingira limeendelea kusimamiwa na kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira safi na salama.

Amesema ushiriki wa wananchi, viongozi na wadau mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha kampeni hiyo inaleta matokeo yanayotarajiwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com