Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI ATEMBELEA CHUO CHA RELI (KORAIL) KOREA KUSINI




Na Mwandishi Wetu, Korea Kusini.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa David Kihenzile, ametembelea Chuo cha Reli cha KORAIL nchini Korea Kusini kwa lengo la kuona namna taasisi hiyo inavyotoa mafunzo kwa wataalamu wa reli pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika uendeshaji wa huduma za usafiri wa reli.

Katika ziara hiyo Mheshimiwa Kihenzile pamoja na masuala mengine alipata wasilisho kutoka kwa Uongozi wa chuo kuhusu programu mbalimbali za mafunzo zinazolenga kuandaa wataalamu wa kada tofauti za reli, zikiwemo uendeshaji wa treni usimamizi wa miundombinu, usalama wa reli na matumizi ya teknolojia za kisasa.

Akizungumza baada ya kutembelea chuo hicho, Mheshimiwa Kihenzile amesema Tanzania inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya reli ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), hivyo uzoefu wa Korea Kusini katika kuandaa na kuendeleza wataalamu wa reli ni muhimu kwa maendeleo ya sekta hiyo nchini.

Vilevile Mheshimiwa Kihenzile ameongeza kuwa Serikali itaendelea kujifunza na kubadilishana uzoefu na taasisi mbalimbali za mafunzo ya reli duniani ili kuongeza uwezo wa wataalamu wa Kitanzania na kuhakikisha uwekezaji unaofanyika katika sekta ya reli unaleta matokeo yaliyokusudiwa.

Aidha Mheshimiwa Kihenzile ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Chuo cha Reli cha KORAIL katika maeneo ya mafunzo, utafiti na kubadilishana uzoefu, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kukuza ujuzi wa wataalamu wa reli na kuimarisha maendeleo ya sekta ya uchukuzi nchini.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com