
Na: Mwandishi wetu - Rukwa
Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkansi, Manispaa ya Sumbawanga na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa, Mhe. Jacqueline Mzindakaya, wameeleza kufurahishwa na jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha huduma za afya, huduma za uchunguzi na matibabu kwa wananchi abavyo vitasaidia kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto, baada ya Zahanati za Chala na King’ombe kupatiwa na Serikali vifaa tiba vyenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 312.
Vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 267 vimetolewa katika Zahanati ya Chala, Wilayani Nkansi, na vyenye thamani ya shilingi milioni 45 vimetolewa katika Zahanati ya King’ombe, Manispaa ya Sumbawanga, kwa lengo la kuongeza uwezo wa vituo hivyo kutoa huduma bora na salama za afya, ikiwepo huduma za afya ya mama na mtoto.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa wananchi kwa niaba ya Serikali, Septemba 30, 2026, Mhe. Mzindakaya amesema uwepo wa vifaa hivyo utaboresha huduma za uchunguzi na matibabu, kuimarisha mazingira ya kazi kwa watumishi wa afya na kuongeza uwezo wa zahanati hizo kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.
“Tumepata vifaa tiba vitakavyotusaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi pamoja na kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto. Ujio wa vifaa hivi unatokana na dhamira ya dhati ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutokomeza vifo vya wanawake wajawazito na watoto nchini,” amesema Mhe. Mzindakaya.
Mhe. Mzindakaya amefafanua kuwa lengo la Serikali kupeleka vifaa hivyo ni kuimarisha upatikanaji wa vifaa muhimu katika vituo vya afya, kuboresha ubora wa huduma, kuimarisha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa afya na kupunguza changamoto zinazotokana na upungufu wa vifaa tiba, hivyo ameishukuru Serikali kwa kutoa vifaa hivyo kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Nkansi na Manispaa ya Sumbawanga.
Miongoni mwa vifaa tiba vilivyotolewa na Serikali kupitia mgao wa Mradi wa TCHMP ni mashine za kupima shinikizo la damu za kidijitali, vifaa vya kupima mapigo ya moyo wa mtoto tumboni, mashine ya kufuatilia hali ya mgonjwa, mashine ya kufuatilia hali ya mgonjwa, seti za vifaa vya kusaidia kujifungua kwa kutumia uvutaji, viti vya magurudumu kwa wagonjwa, friji za kuhifadhia bidhaa za dawa pamoja na vitanda vya kujifungulia.
Utoaji wa vifaa hivyo unaongeza uwezo wa Zahanati za Chala na King’ombe kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na kuweka mazingira bora na salama kwa wananchi wanaohitaji huduma za afya, wakiwepo wanawake wajawazito na watoto.











Social Plugin