Na Regina Ndumbaro Tunduru-Ruvuma
Mfumo wa stakabadhi ghalani umeendelea kuwa tegemeo kwa wakulima wa mbaazi Wilaya ya Tunduru baada ya kuwawezesha kuuza mazao yao kwa uwazi na kupata bei yenye tija, huku wakulima wakisema kuuza nje ya mfumo huo kungeweza kuwaingiza katika hasara.
Kauli hiyo imetolewa na Issa Haji Issa, mkulima kutoka Chama cha Kidompo AMCOS, baada ya kufanyika kwa mnada wa nne wa mbaazi katika Kijiji cha Kidodoma, Tarafa ya Nampungu, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma.
Katika mnada huo uliofanyika kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa kidijitali wa TMX, jumla ya kilo 867,307 za mbaazi zimeuzwa kwa bei ya Sh. 1,412 kwa kilo.
Issa amesema wakulima wameridhishwa na bei hiyo, akieleza kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani umekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha wakulima wanapata bei inayotokana na ushindani wa wanunuzi badala ya kutegemea makadirio ya bei.
“Sisi kama wakulima tumekubali bei hiyo ya 1,412 kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na kama tungeuza nje ya mfumo huu tungepata hasara. Mfumo huu ni mzuri sana kwa mkulima,” amesema.
Amesema tofauti kubwa na utaratibu wa zamani ni uwazi katika mchakato wa mauzo, ambapo mkulima anaweza kufuatilia kinachoendelea wakati wanunuzi wanaposhindana kununua mazao.
“Sisi kwa niaba ya wakulima wenzetu wa Wilaya yote ya Tunduru tumeridhishwa na bei ya mbaazi kwa kuwa ni bei nzuri. Kabla ya mfumo huu tulikuwa tunakadiriwa bei, lakini mfumo huu ni wa uwazi, kila mkulima anaona kila kinachoendelea namna wanunuzi wa mazao wanavyonunua mazao ya mkulima,” amesema.
Kwa mujibu wa Issa, mfumo huo pia umeondoa usumbufu katika upatikanaji wa malipo, kwani wakulima hupata fedha baada ya siku mbili.
Amesema hali hiyo imewapa wakulima uhakika zaidi katika kupanga matumizi ya kipato wanachokipata kutokana na kilimo.
Naye Fatu Rajabu Kalesi, mkulima, amesema mapato anayopata kutokana na mauzo ya mazao kupitia mfumo huo yana mchango mkubwa katika maisha ya familia yake, ikiwemo kusomesha watoto, kuinua uchumi wa familia na kujikimu kimaisha.
Mnada huo umesimamiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Tunduru (TAMCU LTD), ambacho ni mlezi na msimamizi wa shughuli za kilimo zinazofanywa na wakulima, ikiwemo kuwawezesha kupata pembejeo za kilimo, masoko na kusimamia minada kupitia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS).
Kais Rashidi Makolela, Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU LTD), amewataka wafanyabiashara kuwa sehemu ya mafanikio ya wakulima kwa kununua mazao yao kwa bei yenye tija.
Amesema nguvu ya mfumo huo itaendelea kuonekana zaidi iwapo wafanyabiashara wataendelea kushiriki katika minada na kumpa mkulima bei inayoridhisha.
Makolela amesema TAMCU LTD inasimama pamoja na wakulima kuhakikisha wanapata soko la mazao yao, huku akieleza kuwa furaha ya mkulima kuona mazao yake yameuzwa ni sehemu ya mafanikio ya chama hicho.
Dira ya TAMCU LTD ni kuwa Chama Kikuu cha Ushirika kinachoongoza kwa kutoa huduma bora na endelevu kwa wanachama na wakulima wake, ikiwemo kuwawezesha kupata pembejeo bora za kilimo, elimu na ushauri wa kilimo, mikopo yenye riba nafuu, kuongeza thamani ya mazao na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika.
TAMCU LTD imeendelea pia kuwahimiza wakulima kuwa wabunifu ili kuongeza tija na thamani ya mazao yao na hatimaye kuongeza manufaa wanayopata kutokana na kilimo.









Social Plugin