MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Christina Mnzava, amechangia shilingi milioni mbili kwa ajili ya ununuzi wa matenki matatu ya kuhifadhi maji, yenye ujazo wa lita 1,000 kila moja, katika Shule ya Sekondari Zunzuli, iliyopo Kata ya Mwenge, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Mchango huo unalenga kusaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama shuleni hapo, huku ukiboresha mazingira ya kujifunzia na ustawi wa wanafunzi.
Dkt. Mnzava alitoa fedha hizo Septemba 24, 2026, wakati akiwa mgeni rasmi katika Mahafali ya 34 ya Kidato cha Nne yaliyofanyika shuleni hapo.
Akizungumza wakati wa kujibu risala ya shule, Dkt. Mnzava amesema upatikanaji wa elimu bora unapaswa kwenda sambamba na uwepo wa mazingira rafiki na salama ya kujifunzia, ambayo yanawawezesha wanafunzi kujikita kikamilifu katika masomo yao.
Amesema changamoto zinazohusu huduma muhimu, ikiwemo maji, zinapaswa kutatuliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, viongozi, wazazi, wadau wa elimu na jamii kwa ujumla.
Sambamba na hilo, Dkt. Mnzava amewataka wazazi na walezi kuendelea kuwaunga mkono watoto wao wakati na baada ya kuhitimu elimu ya sekondari, akisisitiza umuhimu wa kutowakatisha tamaa kutokana na matokeo au changamoto wanazoweza kukutana nazo.
Amesema kila mtoto ana uwezo na kipaji chake katika nyanja mbalimbali, ikiwemo elimu, michezo na shughuli nyingine za kijamii.
Awali, akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Mkuu wa Shule ya Sekondari Zunzuli, George Elia Ulomi, amesema licha ya Serikali kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo, bado kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Amesema hali hiyo imekuwa ikileta changamoto katika maisha ya kila siku ya wanafunzi na mazingira ya shule kwa ujumla, hivyo msaada wa ununuzi wa matenki hayo utasaidia kuboresha hali hiyo.
Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya wazazi na walezi, Machange Magiga, amewapongeza walimu kwa kuwa mhimili muhimu katika malezi na utoaji wa elimu kwa wanafunzi.
Amesema wazazi wana imani kuwa wahitimu hao watafanya vizuri katika mtihani wao wa kuhitimu elimu ya sekondari, huku akiwataka kuendelea kuwatia moyo na kuwaunga mkono katika hatua zinazofuata za maisha yao.
Katika mwaka wa masomo 2025, Shule ya Sekondari Zunzuli ilishika nafasi ya kwanza katika matokeo ya Kidato cha Nne kwa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ikiwa na jumla ya wanafunzi 98.
Mafanikio hayo yanaendelea kuifanya shule hiyo kuwa miongoni mwa shule zinazofanya vizuri katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, huku uongozi wa shule ukiendelea kusisitiza ushirikiano kati ya walimu, wanafunzi, wazazi na wadau wa elimu katika kuboresha zaidi ufaulu.






Social Plugin