Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Julius S. Mtatiro, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, wakati wa SHYCOM Alumni Half Marathon 2026, iliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kambarage, Manispaa ya Shinyanga. Picha na Stela Paul
Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Rogath John Akhwari, akizungumza wakati wa SHYCOM Alumni Half Marathon 2026, iliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kambarage, Manispaa ya Shinyanga.
Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya SHYCOM Alumni Half Marathon 2026, Josta Dominick, akizungumza wakati wa mbio hizo zilizofanyika katika Uwanja wa CCM Kambarage, Manispaa ya Shinyanga.
Na Stela Paul - Shinyanga
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ameahidi kuwa Serikali mkoani humo itaendelea kutoa ushirikiano kwa waandaaji wa SHYCOM Alumni Half Marathon 2026, ili kuhakikisha mbio hizo zinaendelea kuwa chachu ya kuimarisha afya ya jamii na kuchangia maendeleo ya Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM).
Mhe. Mhita ametoa ahadi hiyo leo, Septemba 26, 2026, kupitia Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, aliyemwakilisha katika mashindano ya SHYCOM Alumni Half Marathon 2026, yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kambarage, Manispaa ya Shinyanga.
Mashindano hayo yamefanyika kwa mara ya pili tangu kuanzishwa kwake, yakiwa na lengo la kuhamasisha jamii kushiriki katika michezo kwa ajili ya afya, huku pia yakichangisha fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Chuo cha Ualimu Shinyanga.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Wakili Mtatiro amesema Serikali ya Mkoa wa Shinyanga inatambua mchango wa mbio hizo katika kuunganisha michezo, afya na maendeleo ya elimu, hivyo itaendelea kushirikiana na waandaaji katika utekelezaji wa shughuli zao.
“Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, nawapongeza wote mlioshiriki mashindano haya, pamoja na wenzetu ambao kwa msimu wa pili mfululizo wanaendesha riadha hii. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ameelekeza kwamba mamlaka za Mkoa wa Shinyanga zitaendelea kuwapatia ushirikiano katika kila jambo watakalohitaji,” amesema Wakili Mtatiro.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Rogath John Akhwari, amesema SHYCOM Alumni Half Marathon imeendelea kuwa moja ya majukwaa yanayoweza kuchangia katika kuibua na kukuza vipaji vya riadha kutoka Shinyanga na maeneo mengine nchini.
Amesema kupitia mashindano hayo, wanariadha wanapata fursa ya kushiriki katika mazingira ya ushindani na hatimaye kuwakilisha Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
“Lazima tujivunie wanariadha kutoka kwenye mkoa wetu hapa. Moja kati ya kazi kubwa inayofanywa na SHYCOM Marathon ni kuzalisha wanariadha hapa nchini na leo wanatuwakilisha kimataifa,” amesema Akhwari.
Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya SHYCOM Alumni Half Marathon 2026, Josta Dominick, amesema lengo la mbio hizo mwaka huu ni kuendeleza juhudi za kuimarisha afya ya jamii huku sehemu ya mapato ikielekezwa katika kuboresha miundombinu ya Chuo cha Ualimu Shinyanga.
Dominick amesema waandaaji wameendelea kuendesha mbio hizo kama mbio za hisani, wakiamini kuwa michezo inaweza kuwa nyenzo ya kuunganisha wahitimu wa SHYCOM, wanafunzi, wananchi na wadau mbalimbali katika kuchangia maendeleo ya chuo hicho.
“Lengo na madhumuni ya marathon hii kwa mwaka huu ni kuendelea kuchochea juhudi endelevu za kuimarisha afya ya jamii na kuchangia maendeleo ya miundombinu ya Chuo cha Ualimu Shinyanga,” amesema Dominick.
Aidha, Dominick amewataka wadau mbalimbali, zikiwemo taasisi, makampuni, wafanyabiashara na wananchi wenye mapenzi mema, kuendelea kushirikiana na waandaaji ili kuhakikisha malengo ya mbio hizo yanafikiwa.
Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuendeleza juhudi za kuboresha mazingira ya elimu na kuchangia ustawi wa jamii mkoani Shinyanga na Tanzania kwa ujumla.

Katika kuunga mkono juhudi hizo za kuboresha mazingira ya wanafunzi, Benki ya CRDB imekabidhi vitanda 20 vya ghorofa mbili (double decker) vyenye uwezo wa kulaza wanafunzi 40 katika Chuo cha Ualimu Shinyanga.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kaimu Meneja wa CRDB Bank Kanda ya Magharibi, Evodi Kereti, amesema mchango huo ni sehemu ya juhudi za Benki ya CRDB kuunga mkono Serikali pamoja na SHYCOM Alumni katika kuboresha mazingira ya wanafunzi, huku akiwashukuru wahitimu hao kwa kuendelea kuwa wateja wa benki hiyo.
Aidha, Benki ya CRDB imeahidi kuendelea kuwa mdau wa karibu wa SHYCOM Alumni Half Marathon na kushiriki katika jitihada zinazolenga kuleta matokeo chanya kwa chuo na jamii kwa ujumla.


































































































Social Plugin