Nzega, Tabora
Mkurugenzi Mtendaji wa Mashili Company Limited Ndg Peter Mashili, Leo tarehe 29 Septemba, 2026 ametekeleza ahadi aliyoitoa Agosti 7, 2026 wakati alipokuwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya Nne ya Chuo cha Uuguzi na Ukunga Nzega, kwa kukabidhi kichomea taka (incinerator) alichokijenga kwa gharama ya shilingi Milioni 6.9 pamoja na jenereta ambalo amelinunua shilingi milioni 4.2, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na utoaji wa mafunzo chuoni hapo.
Akikabidhi mchango huo leo Septemba 29, 2026 kwa Mkuu wa Chuo cha Uuguzi na Ukunga Nzega, Bw. Josephat K. Kaja, Mashili amesema utekelezaji wa ahadi hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha elimu na mafunzo ya wataalamu wa afya, sambamba na kuboresha mazingira ya wanafunzi na wakufunzi.
Mashili amesema vifaa hivyo vyote vilivyogharimu shilingi milioni 11.186 ili ni maalumu kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za umeme na kuboresha mazingira ya chuo.
Amesema kichomea taka kitasaidia kuboresha usimamizi wa taka zinazozalishwa katika mazingira ya chuo, hususani taka zinazohusiana na mafunzo na huduma za afya, wakati jenereta litasaidia kuhakikisha shughuli za mafunzo zinaendelea hata pale kunapokuwa na changamoto ya upatikanaji wa umeme.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Nzega, Bi Zalna Dickolagwa, amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Mashili Company Limited Ndg Peter Mashili kupitia kampuni yake inayojihusisha na uchimbaji wa madini kwa kuendelea kufanya shughuli za uwekezaji huku akitambua umuhimu wa kurudisha sehemu ya mafanikio kwa jamii kupitia Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Amesema utekelezaji wa ahadi hiyo umeongeza uaminifu kwa wananchi, kwa kuwa Mashili ameonesha kwa vitendo kwamba ahadi anazotoa anazitekeleza.
Amesema Serikali wilayani Nzega itaendelea kushirikiana na Mashili Company pamoja na sekta binafsi kwa ujumla, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuchochea utekelezaji wa shughuli za maendeleo zitakazonufaisha jamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Uuguzi na Ukunga Nzega, Bw. Josephat K. Kaja, amemshukuru Mashili kwa kutekeleza ahadi hiyo, akisema msaada huo utasaidia kukabiliana na changamoto zilizokuwa zikiathiri mazingira ya kujifunzia na uendeshaji wa shughuli za chuo.
Mchango huo unakuja ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kuongeza idadi ya wataalamu wa afya nchini kupitia vyuo vya mafunzo, wakati Chuo cha Uuguzi na Ukunga Nzega kikiwa na wanafunzi 143, wakiwemo wasichana 93 na wavulana 50.












Social Plugin