Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MANTRA TANZANIA YAONGEZA MIRADI YA MAENDELEO KWA JAMII LIKUYU

Kituo cha Afya Likuyu kilichojengwa na kampuni ya MANTRA Tanzania Ltd kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa Kijiji hicho kupata huduma za matibabu kwa haraka ambacho bado kinaendelea na ujenzi 
Meneja  Mahusiano wa kampuni ya MANTRA Tanzania Ltd Manace Ndoroma akiwa anazungumza na wananchi wa Kijiji cha Likuyu baada ya kupewa nafasi na Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt.Juma Zuberi Homera akielezea miradi waliyoitoa kwa wananchi na miundombinu mingine inayoendelea 
Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt.Juma Juma Zuberi Homera akiwa mwenye furaha baada ya kuona wananchi wa jimbo lake wakiridhishwa na kile anachokifanya hasa utekelezaji wa miradi mbalimbali aliyoiahidi kwa wananchi wake

Na Regina Ndumbaro

Namtumbo-Ruvuma

Kampuni ya Mantra Tanzania Limited, inayotekeleza Mradi wa Mkuju River Uranium katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, imeendelea kushirikiana na jamii ya Likuyu kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu, maji na huduma za jamii. 

Hayo yameelezwa wakati wa ziara ya Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, katika eneo hilo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Meneja Mahusiano wa Mantra Tanzania Limited, Manace Ndoroma, amesema kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana vizuri na wananchi wa Likuyu na kwa mwaka 2026/2027 imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali. 

Amesema miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa nyumba ya mwalimu katika Shule ya Msingi Muungano pamoja na kuendelea na ujenzi wa miundombinu katika Kituo cha Afya Likuyu.

Ndoroma amesema katika Kituo cha Afya Likuyu wanajenga nyumba mbili za watumishi ili kuwawezesha wataalamu hao kuishi karibu na kituo na hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma muda wote. 

Aidha, amesema kampuni hiyo inajenga mnara wa tenki la maji kwa kuwa tayari maji yamefika katika eneo hilo na yanahitaji kupandishwa juu ili yaweze kufikika kwa urahisi zaidi.

Ameongeza kuwa Mantra Tanzania Limited inajenga vyoo vitano katika eneo la shule, ambavyo viwili vitatumika na wanaume, viwili wanawake na kimoja kwa ajili ya watu wenye ulemavu, pamoja na kujenga sehemu za kunawia mikono na mashimo ya taka nyepesi na taka ngumu. 

Amesema lengo ni kuhakikisha kituo kinaanza kutoa huduma huku ujenzi wa miundombinu mingine ukiendelea.

Kwa upande wake, Dkt. Juma Zuberi Homera ameupongeza uongozi wa Mantra Tanzania Limited kwa kushirikiana na jamii ya Namtumbo na kutekeleza miradi hiyo, huku akiwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano. 

Wananchi wa Likuyu, Hadija Ismail Mtamila na Kaisi, kwa niaba ya wanakijiji, wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Juma Zuberi Homera pamoja na Mantra Tanzania Limited kwa kuwajali na kusaidia kutatua changamoto za muda mrefu kupitia miradi ya afya, elimu, maji na miundombinu mingine.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com