Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KIGAILA APOKEA WANACHAMA WAPYA ZAIDI YA 300 CHAUMMA BAHI



Na mwandishi wetu,Dodoma

KATIBU Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Benson Kigaila, amepokea wanachama wapya zaidi ya 300 kutoka Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma, walioamua kujiunga na chama hicho.

Wanachama hao wamekabidhiwa kadi za uanachama na Kigaila leo Septemba 22,2026 katika Kijiji cha Mpinga, Kata ya Mpinga, Wilaya ya Bahi.

Kigaila alikuwa ameambatana na Mkurugenzi wa Bunge, Halmashauri na Tawala za Mikoa wa Chaumma, Kayombo Kabutal, pamoja na Katibu wa Chaumma Mkoa wa Dodoma, Mathias Nyakapala.

Akizungumza na wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Kigaila alisema hali ya umaskini inayowakabili baadhi ya wananchi wa Bahi imesababishwa na kuendelea kukichagua Chama cha Mapinduzi (CCM).

Alisema wakati umefika kwa wananchi hao kufanya mabadiliko ya kisiasa kwa kuondoa CCM madarakani na kukipa nafasi Chaumma, akieleza kuwa chama hicho kinaamini kinaweza kuleta maendeleo ambayo wananchi wa Bahi wamekuwa wakiyahitaji kwa muda mrefu.

“Nyinyi ni maskini wa kutupa kwa sababu ya kuichagua CCM. Wamewatelekeza na ninyi mpo tu, maisha yenu hayaeleweki. Hebu jitathmini, achaneni na CCM sasa, chagueni Chaumma,” alisema Kigaila.

Kwa upande wake, Kabutal alisema pamoja na Wilaya ya Bahi kuwa na utajiri wa rasilimali za madini ikiwemo Uranium, wananchi wake bado wameendelea kukabiliwa na hali ya umaskini.

Kutokana na hali hiyo, aliwaomba wananchi wa Bahi kukiamini Chaumma na kukipa nafasi ya kushiriki katika uongozi ili kutekeleza sera na mipango yake ya maendeleo.

Naye Novatus Madanya, mmoja wa wanachama wapya waliojiunga na Chaumma, alisema ameamua kuunga mkono chama hicho kutokana na kuridhishwa na sera zake.

Alisema anaamini sera hizo zinaweza kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi wa Bahi.

Kwa upande wake, Neema Mlay alisema wananchi wa Bahi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa maji kwa muda mrefu.

Mlay alisema hali hiyo imewafanya baadhi ya wananchi kuhisi kama wametelekezwa na kunyanyaswa licha ya kuwa sehemu ya nchi yenye rasilimali mbalimbali.

Alisema wananchi wanahitaji kuona mabadiliko katika huduma za msingi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuboresha maisha yao.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com