Na Marco Maduhu, SHINYANGA
BADSON Mining Consultation & Foundation imezindua rasmi huduma ya kuwaunganisha wafursa katika sekta ya madini na wawekezaji, kwa lengo la kusaidia kukuza uwekezaji katika sekta hiyo nchini Tanzania.
Huduma hiyo imezinduliwa leo Septemba 11, 2026, ikiwa na dhamira ya kuwa daraja la kuwaunganisha wamiliki wa maeneo ya madini, wataalamu, wataalamu wa sekta hiyo na wawekezaji wa ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza wakati wa kuzindua Kampuni hiyo Katibu Tawala wa wilaya ya Kahama Glory Absalum akimwakiklisha Mkuu wa wilaya hiyo Frank Nkinda, ameipongeza Kampuni hiyo, kwamba inakwenda kuwa msaada mkubwa kwa wachimbaji wadogo ikiwamo namna ya kumiliki leseni na kuondokana na migogoro ya kugombania maeneo.
Amesema, migogoro mingi katika sekta ya madini mara nyingi imekuwa ikitokana na ukosefu wa elimu kuhusu uwekezaji katika sekta hiyo, na kuwataka wachimbaji wadogo wa madini kufika katika kampuni hiyo na kupata ushauri mbalimbali kabla ya kuwekeza kwenye sekta hiyo.
“Nakupongeza kwanza Mkurugunzi wa Badson Mining kwa uwekezaji mkubwa ambao umeufanya hapa Kahama sisi kama serikali tutakupatia ushirikiano wa kutosha, sababu Kahama kuna migodi mingi ya madini na utakuwa msaada mkubwa kwetu,” amesema Absalum.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Badson Mining Consultaion Richard Kayangu, amesema, taasisi hiyo imeanzishwa kutokana na msisitizo mkubwa katika madini ya dhahabu, huku ikilenga kupanua wigo wake katika fursa nyingine zinazopatikana kwenye sekta ya madini nchini.
Dhima ya Badson
Taasisi hiyo, imeeleza kuwa inalenga kusaidia kupunguza pengo kati ya watu wenye fursa katika sekta ya madini, na wale wenye uwezo na nia ya kuwekeza.
Richard amesema, watakuwa wakitoa ushauri, elimu, mwongozo na mtandao wa wataalamu na wadau, ili kusaidia kuwaunganisha wamiliki wa fursa za madini na wawekezaji.
Ametaja miongoni mwa majukumu yake, ni kuwaunganisha wamiliki wa fursa za madini na wawekezaji, kutoa ushauri na kusaidia kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.
Pia, Badson inalenga kutoa ushauri, elimu na mwongozo kwa wanaotaka kuingia katika sekta ya madini, pamoja na kuwaunganisha wataalamu wa wawekezaji na wadau ndani na nje ya Tanzania.
Aidha, taasisi hiyo imeeleza kuwa itawasaidia wadau kupata taarifa muhimu kwa ajili ya kufanya maamuzi ya uwekezaji, huku ikihakikisha uwekezaji unazingatia sheria, taratibu, uwajibikaji na mazingira.
Amesema, pia Badson kutakuwa na fursa mbalimbali katika sekta ya madini ikiwamo kujumuisha huduma za kitaalamu, teknolojia, vifaa, usafirishaji, biashara na shughuli nyingine zinazohusiana na sekta hiyo.
Kupitia huduma hiyo, Badson Mining Consultation & Foundation, inalenga kuongeza uelewa wa vijana na jamii kuhusu fursa zinazopatikana katika sekta ya madini.
Dira
Taasisi hiyo imeeleza kuwa dira yake ni kujenga taasisi inayotambulika kama daraja la kuunganisha fursa, taarifa, utaalamu na mitaji katika sekta ya madini.
Aidha, imeeleza kuwa haitoi dhamana ya mafanikio ya uwekezaji, bali inasaidia wadau kupata taarifa, mwongozo, mitandao na wataalamu wanaohitajika ili kufanya maamuzi yenye uelewa.
“Tunataka kujenga daraja kati ya fursa za madini na watu wenye uwezo na nia ya kuwekeza. Tunataka fursa ziwe fursa kwa watu sahihi, na wawekezaji wapate taarifa na mwongozo unaohitajika kabla ya kuchukua hatua,”amesema Richard.
Katika hatua nyingine amesema Kampuni hiyo itakuwa ikisaidia watu wenye uhitaji kama sehemu ya kurudisha faida.
TAZAMA PICHA👇👇
Katibu Tawala wa wilaya ya Kahama Glory Absalum akizungumza.
Katibu Tawala wa wilaya ya Kahama Glory Absalum (kulia)akikata Utepe kuzindua Kampuni ya Madini ya Badson, kushoto ni Mkurugenzi wa Badson Mining Richard Kanyangu.
Katibu Tawala wa wilaya ya Kahama Glory Absalum (kulia) akimlisha Keki Mkurugenzi wa Badson Mining Richard Kanyangu kwenye uzinduzi wa Kampuni hiyo.
Mkurugenzi wa Badson Mining Richard Kanyangu (kushoto) akimlisha keki Katibu Tawala wa wilaya ya Kahama Glory Absalum kwenye uzinduzi wa kampuni hiyo.
Social Plugin