Bweni la wavulana la shule ya Sekondari Chandarua lililokuwepo katika moja ya mradi katika ilani ya chama cha mapinduzi CCM Kata ya Mshangano jimbo la Songea mjini linalogharimu kiasi cha shilingi milioni 150 lenye uwezo wa kulala wavulana 80 kwenye mabweni hayoNa Regina Ndumbaro, Songea-Ruvuma
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mshangano, jimbo la Songea mjini imefanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika kata hiyo, ikiwa ni pamoja na Bweni la wavulana la shule ya sekondari Chandarua, maabara ya kisasa ya shule hiyo, shule ya msingi Luhila pamoja na ukumbi wa mikutano katika shule ya msingi Chifu Zulu, kwa lengo la kujiridhisha namna miradi hiyo inavyoendelea na matumizi ya rasilimali zilizotengwa.
Ziara hiyo imekuja wakati Kata ya Mshangano ikieleza utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo katika kipindi cha Oktoba 2025 hadi Septemba 2026, ambapo zaidi ya Sh. milioni 998.87 zimetajwa kuelekezwa katika maeneo mbalimbali, yakiwemo elimu, afya, utawala na uwezeshaji wa vikundi vya wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani iliyowasilishwa na Diwani wa Kata ya Mshangano, Benson J. Sovella, Sh milioni 720.87 zilitengwa kwa miradi ya elimu, Sh. milioni nne kwa miradi ya afya na Sh. milioni 270 kwa miradi ya utawala.
Katika sekta ya elimu, taarifa hiyo inaeleza kuwa utekelezaji umehusisha ujenzi na ukarabati wa miundombinu pamoja na upatikanaji wa samani, ambapo jumla ya madawati, viti na meza 298 zimetengenezwa kwa ajili ya shule za msingi na sekondari.
Kata hiyo ina jumla ya shule 13 za msingi, zikiwemo tisa za serikali na nne zinazomilikiwa na watu binafsi au mashirika, pamoja na shule saba za sekondari, ambazo mbili ni za serikali na tano ni za watu binafsi au mashirika.
Aidha, katika sekta ya maji, huduma imefikia takribani asilimia 85 ya kata yenye mitaa mitano, huku mitaa minne kati ya mitano ikiwa imefikiwa na huduma ya umeme.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mshangano Ahmad Yahaya Nawanje amewataka wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kusimamia kikamilifu miundombinu iliyojengwa ili kuzuia uvunjifu, uharibifu au uchakavu wa maeneo hayo.
Msisitizo huo umetolewa katika ziara ambayo pia imehusisha maeneo yenye miradi ya elimu, wakati kata hiyo ikiwa na wakazi 22,042 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, idadi inayoongeza umuhimu wa miundombinu bora na inayotunzwa kwa ajili ya huduma kwa wananchi.
Mbali na elimu, taarifa ya utekelezaji inaonyesha kuwa kata imeendelea kugusa maeneo ya afya, maji, nishati, kilimo na uwezeshaji wa wananchi, ambapo vikundi 12 vya kijamii na kiuchumi vimeundwa na kusajiliwa; vikundi sita vya wanawake vilipatiwa Sh milioni 19, huku kikundi kimoja cha vijana chenye vijana watano kikipewa pikipiki tano zenye thamani ya Sh milioni 16.535.
Kwa mtazamo wa utekelezaji huo, ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Kata ya Mshangano imeweka mkazo katika kufuatilia hali ya miradi iliyotekelezwa na kusisitiza wajibu wa wasimamizi kuhakikisha miundombinu hiyo inalindwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.






Social Plugin