Na Sumai Salum-Kishapu
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, amewataka askari wa Jeshi la Akiba wilayani humo kutumia mafunzo waliyopata katika kuimarisha utayari wa jamii kukabiliana na majanga mbalimbali, ikiwemo athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño.
Mhe. Masindi ametoa rai hiyo leo Septemba 30, 2026, wakati alipokutana na askari wa Jeshi la Akiba baada ya kukamilika kwa mafunzo ya utayari wa kukabiliana na majanga yaliyohusisha makundi mbalimbali katika wilaya hiyo.
Amesema Jeshi la Akiba lina nafasi muhimu katika kusaidia Serikali kujenga jamii yenye uelewa na utayari wa kukabiliana na majanga, hivyo amewataka askari hao kuwa mabalozi wa elimu ya tahadhari za majanga katika maeneo yao.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi akizungumza na askari hao wa jeshi la akiba wilayani humo septemba 30, 2026
“Tunataka mafunzo haya yaonekane katika vitendo. Kila mmoja wenu akawa sehemu ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na majanga, kuchukua tahadhari mapema na kushirikiana na mamlaka pindi yanapotokea,” amesema Mhe. Masindi.
Aidha, amewataka askari hao kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira, ikiwemo kuondoa taka na vitu vinavyoweza kuziba mifereji ya maji, pamoja na kuchukua tahadhari katika maeneo hatarishi wakati wa mvua.
Amesema utayari wa kukabiliana na majanga haupaswi kuachiwa Serikali pekee, bali unahitaji ushirikiano wa wananchi, viongozi, taasisi na makundi mbalimbali katika jamii ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Katibu Tawala wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Fatma Mohamed
Kwa upande wake, Kaimu Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Kishapu, CAPT MS Mhina amesema Jeshi la Akiba litaendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu utayari wa kukabiliana na majanga pamoja na kulinda mazingira.
"Jeshi la Akiba litaendelea kuwa tayari kuitikia wito wa Serikali wakati wowote linapohitajika, hususan katika shughuli za uokoaji na kukabiliana na majanga, huku likishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi" amesema CAPT Mhina.
Amesema mafunzo hayo yamewaongezea uwezo na uelewa wa namna ya kuchukua hatua za haraka wakati wa majanga, kutoa elimu ya tahadhari kwa jamii na kusaidia kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na majanga mbalimbali.
Kaimu Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Kishapu, CAPT MS Mhina
Aidha, amewataka askari wa Jeshi la Akiba kutumia maarifa waliyopata kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujiandaa na kuchukua tahadhari dhidi ya mvua za El Niño, kutunza mazingira, pamoja na kutoa taarifa mapema pale wanapoona viashiria vya hatari katika maeneo yao.
Amesisitiza kuwa Jeshi la Akiba ni sehemu muhimu ya jamii, hivyo askari wanapaswa kuendelea kudumisha nidhamu, uzalendo, utii, umoja na ushirikiano, huku wakiwa mfano bora katika maeneo wanayoishi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na usalama wa jamii.
Afisa Uhamiaji wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Cecilia Lucas Matoboki
Social Plugin