Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT. MWIGULU AAGIZA MFUMO MPYA WA UNUNUZI PAMBA UWE TAYARI NDANI YA MWEZI MMOJA


Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemuagiza Waziri wa Kilimo kukutana na wadau wa zao la pamba na ndani ya mwezi mmoja kuwasilisha mapendekezo ya mfumo bora wa ununuzi wa pamba utakaowanufaisha wakulima na kuchochea uzalishaji wa zao hilo nchini.


Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo, Jumatatu Septemba 14, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa Itilima mkoani Simiyu, baada ya Mbunge wa Itilima, Mhe. Njalu Daudi Silanga, kuwasilisha changamoto zinazowakabili wakulima wa pamba, ikiwemo malalamiko kuhusu mfumo wa sasa wa ununuzi wa zao hilo.

“Leo tarehe 14, mpaka tunapofika tarehe 14 mwezi ujao, niwe nimeshapata taarifa ya utaratibu mzuri ambao tutakubaliana,” amesema Dkt. Mwigulu.

Amesema Serikali italinganisha mifumo iliyowahi kutumika katika ununuzi wa pamba na mfumo unaotumika sasa, ili kubaini utaratibu utakaokuwa na manufaa zaidi kwa wakulima, huku ukilinda uzalishaji, bei ya pamba na maisha ya wananchi wanaotegemea zao hilo.

Akizungumzia masuala mengine yanayowagusa wananchi, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imeondoa sheria iliyokuwa ikiruhusu mifugo ya wananchi kutaifishwa na kuelekeza kufanyiwa mapitio kwa sheria na kanuni nyingine zinazohusiana na mifugo. Aidha, ameagiza wananchi ambao mifugo yao ilitaifishwa na baadaye wakashinda kesi mahakamani kulipwa stahiki zao.

Waziri Mkuu pia amesisitiza kuwa vyombo vya Serikali havipaswi kuchukua bodaboda, bajaji, baiskeli, mikokoteni au mali nyingine zinazotumiwa na wananchi kujipatia kipato kwa ajili ya kukusanya faini, bali faini zitozwe kwa mujibu wa sheria bila kumnyang’anya mwananchi chombo chake cha kazi.

Kuhusu bei ya saruji, amesema Serikali imeanza kuchukua hatua baada ya kubaini bei kufikia Sh27,000, Sh30,000 na Sh32,000 katika baadhi ya maeneo, huku wataalamu wakipewa wiki moja kuandaa mpango wa kimkakati wa kukabiliana na hali hiyo.

Aidha, Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa mgonjwa anayehitaji rufaa hapaswi kuombwa fedha kwa ajili ya mafuta ya gari la wagonjwa, akielekeza huduma hiyo kutolewa kwa haraka mara baada ya mgonjwa kuandikiwa rufaa.

“Kuanzia sasa mgonjwa asiombwe fedha ya kujaza mafuta kwenye gari la wagonjwa. Mkishamwandikia anahitaji rufaa, mtimizeni, mkimbizeni haraka,” amesema.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali imeelekeza zaidi ya Sh1.4 trilioni katika Mkoa wa Simiyu katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya umeme, barabara, maji, elimu na afya.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, amesema Serikali inaendelea kushughulikia changamoto zinazotokana na mwingiliano kati ya shughuli za wananchi na wanyamapori, ikiwemo kushughulikia madai ya fidia kwa wananchi walioathiriwa na wanyamapori.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Dkt. Festo John Dugange, amesema Serikali inatambua upungufu wa watumishi wa afya na elimu katika Wilaya ya Itilima, akieleza kuwa katika siku 100 za mwanzo za Serikali ya Awamu ya Sita, wilaya hiyo imepata watumishi 51 wa afya na walimu 135.

Amesema Itilima pia imepewa kipaumbele katika vibali vya ajira vitakavyotolewa kwa watumishi wa afya, elimu na kada nyingine.

Kwa upande wake, Mbunge wa Itilima, Mhe. Njalu Daudi Silanga, amesema wilaya hiyo imeendelea kupata uwekezaji katika sekta za elimu, afya, maji, barabara na umeme, huku akiwasilisha changamoto zinazoendelea kuhitaji hatua za Serikali.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com