Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC KISHAPU AHIMIZA JAMII KUTOPUUZA MAANDALIZI YA KUKABILIANA NA EL NINO


Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi

Na Sumai Salum- Kishapu

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi amewataka Afisa Mazingira, Afisa Afya na Afisa Biashara, kuhakikisha wanatimiza majukumu yao ipasavyo wakati nchi ikiendelea na mikakati ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Nino.


Ametoa agizo hilo leo, Septemba 26, wakati wa zoezi la usafi katika Stendi ya Mabasi ya Isoso, wilayani Kishapu. Mkuu huyo wa Wilaya amewaonya wafanyabiashara wasiofanya usafi katika maeneo yao ya biashara, huku akiwaagiza maafisa hao kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.


"Tunahitaji kuchukua hatua sasa ili kuzuia maafa yasije yakawa makubwa. Hakikisheni mitaro yote inazibuliwa, mashimo yanafukiwa na maeneo yanayoweza kusababisha maji kutuama yanafanyiwa usafi. Kila mmoja atimize wajibu wake kwa wakati," amesema.


Aidha, amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi, hususan mabondeni, kuchukua tahadhari mapema na kuhamia maeneo salama. Pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha nyumba zisizo salama, kulinda watoto na wazee, kutunza nyaraka na vitambulisho sehemu salama pamoja na kuhakikisha mifugo inahamishiwa sehemu zisizo na hatari ya mafuriko.


"Hatupaswi kusubiri mvua zianze ndipo tuchukue hatua. Wananchi waendelee kufuatilia taarifa na maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika, waepuke kuvuka mito au madaraja yaliyofunikwa na maji, na watoe taarifa mapema wanapoona dalili zozote za hatari," ameongeza.


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Jacobo Ngainayo, amesema Halmashauri tayari imeandaa mpango shirikishi unaoanzia ngazi ya Vitongoji, Vijiji, Kata hadi Wilaya. Mpango huo pia umehusisha sekta binafsi ili kuimarisha ushirikiano na Serikali katika kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.


Amesema kwa sasa Halmashauri ipo katika hatua ya utekelezaji na inaendelea na kazi mbalimbali za maeneo ya miradi ili mvua nyingi zitakapoanza, kazi nyingi zitakazokuwa zimebaki ziwe zile zinazoweza kufanyika ofisini.


"Katika maeneo yenye miradi, Mhe. Mkuu wa Wilaya, tayari tumehakikisha vifaa vyote vya ujenzi vinapelekwa mapema. Mvua zitakapoanza, hatutaki kukumbana na changamoto ya kushindwa kuyafikia maeneo ya miradi na kuchelewesha huduma ambazo wananchi wanatarajia kuzipata," amesema Ngainayo.


Kuhusu changamoto ya daraja lililoharibika katika Kata ya Itilima, Ngainayo amesema gharama za kulijenga ni kubwa. Hata hivyo, Halmashauri kwa kushirikiana na TARURA imeanza kutengeneza barabara mbadala ili kuhakikisha wananchi hawaathiriki kwa kukosa huduma muhimu.


Diwani wa Kata ya Kishapu, Jole Ndettoson, amesema baadhi ya maeneo yana nyumba za udongo "Tembe", ambazo si imara wala salama kwa wakazi wake. Amesema viongozi wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuzikarabati nyumba hizo na kuhamishia mifugo katika maeneo salama.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Isoso, Robert Nyahuma, amesema baadhi ya wananchi wanaoishi mabondeni katika mitaa anayoisimamia wameanza kuhamia maeneo salama. Ameongeza kuwa wananchi wenye nyumba zisizo salama wanaendelea kuzifanyia ukarabati ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa mvua nyingi.
Katibu Tawala wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Fatma Mohamed
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Jacobo Ngainayo
Diwani wa Kata ya Kishapu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Joel Ndettoson

Afisa mazingira Halamashauri ya Wilaya Kishapu mkoani Shinyanga Cassim Said

Mwenyekiti wa Mtaa wa Isoso Kata ya Kishapu Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Robert Nyahuma






































































Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com