Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DARAJA JIPYA LA LUEGU KUBADILI USAFIRI NAMTUMBO, SERIKALI YAWEKEZA SH.BILIONI 6.1

Daraja la Luegu lililopo kata ya Mgombasi wilayani Namtumbo ambalo Serikali imewekeza kiasi cha shilingi bilioni 6.1 kwaajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa daraja hilo pamoja na barabara za maungio kwa kiwango cha lami 

Na Regina Ndumbaro, Namtumbo-Ruvuma

Wananchi wa Kata ya Mgombasi na maeneo mengine ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wanatarajia kuondokana na adha ya usafiri wakati wa mvua baada ya Serikali kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa daraja jipya la Luegu pamoja na barabara za maungio kwa kiwango cha lami.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 40.8 na barabara za maungio zenye urefu wa kilometa 2.125 katika barabara ya Naikesi-Kitanda. Mkataba wa ujenzi wenye thamani ya Sh.bilioni 6.149,983,643 umesainiwa kati ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma na Kampuni ya Ovans Construction Ltd, huku hafla hiyo ikishuhudiwa na Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Dkt. Juma Zuberi Homera.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini, Dkt. Homera amesema ujenzi wa daraja hilo utasaidia kuondoa kero iliyokuwa ikiikabili jamii kutokana na eneo hilo kujaa maji wakati wa mvua, hali inayosababisha barabara kufungwa na kuwafanya wananchi kushindwa kusafiri kwa urahisi. 

Amesema Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha hizo kwa ajili ya kujenga daraja la kudumu litakalosaidia kuokoa maisha na kuboresha huduma za usafiri.

Dkt. Homera amewataka wananchi kuendelea kuiamini Serikali na kumpa ushirikiano mkandarasi ili mradi huo ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaokusudiwa. 

Aidha, amesema Serikali tayari imeridhia ujenzi wa barabara ya Mtonya-Kitanda kwa kiwango cha lami, hatua ambayo amesema itarahisisha usafirishaji wa mazao kutoka mashambani kwenda mjini na kwenye masoko.

“Jitihada zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan zinaonekana na ametoa zaidi ya Sh.bilioni 6 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 2. Baada ya miezi 12 kama mkataba unavyotaka, sina wasiwasi na uwezo wa mkandarasi wetu,” amesema Dkt. Homera.

Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Ferdinand Mdoe, amesema mradi huo utatekelezwa kwa muda wa miezi 12 na ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha miundombinu ya barabara kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Mhandisi Mdoe amesema daraja lililopo limejengwa zaidi ya miaka 40 iliyopita na wakati wa mvua kubwa maji hufurika na kupita juu ya daraja, hali inayokwamisha shughuli za uzalishaji. 

Amesema daraja hilo pia limechakaa na kuwa dhaifu, hivyo ujenzi wa jipya utasaidia kupunguza hatari za ajali, hususan katika maeneo ya kona za maingilio.

Kwa mujibu wa Mdoe, mradi huo utahusisha ujenzi wa daraja la mita 40.8, boksi kalavati, kunyanyua tuta la barabara upande wa Mtonya, kukata mlima upande wa Naikesi, kujenga barabara za maingilio kwa kiwango cha lami, kuweka taa 20 za barabarani, mifereji ya kupitisha maji, alama za barabarani pamoja na miundombinu mingine.

Amesema mradi huo unafadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania, huku usanifu ukifanywa na Kampuni ya Luptan Consults Ltd na usimamizi ukifanywa na TANROADS Mkoa wa Ruvuma.

Mdoe amesema kutokana na mahitaji ya kibajeti, mradi huo utatekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa daraja, huku awamu ya pili ikihusisha ujenzi wa boksi kalavati, mifereji ya zege, barabara unganishi kwa kiwango cha lami, kazi saidizi za barabara, usimikaji wa taa, uhamishaji wa miundombinu na udhibiti wa ubora.

Kwa upande wake, Mkandarasi wa mradi huo, Valence Urio, amempongeza Dkt. Homera kwa jitihada zake za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo na kuahidi kutekeleza kazi hiyo kwa wakati na kwa ubora kulingana na masharti ya mkataba.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com