
Benki ya CRDB imekabidhi jumla ya madawati 40 kwa Shule ya Msingi Ushetu iliyopo Wilaya ya Mbogwe, Mkoa wa Geita, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni yake ya “Keti Jifunze” inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika shule za umma.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Septemba 29,2026 katika shule hiyo, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbogwe, Adestino Mwilinge kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Sakina Mohamed.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wambura Wagana, amesema utoaji wa madawati hayo ni sehemu ya mwendelezo wa juhudi za benki hiyo kupitia kampeni ya Keti Jifunze, inayolenga kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora na salama ya kujifunzia.
Amesema katika Mkoa wa Geita, CRDB imeendelea kugusa maeneo mbalimbali kupitia kampeni hiyo, ambapo kwa mwaka huu tayari imefikia Wilaya za Chato, Bukombe na Mbogwe.
Wagana amesema CRDB itaendelea kushirikiana na Wilaya ya Mbogwe na kuunga mkono juhudi za maendeleo, hasa kutokana na wananchi wa eneo hilo kuendelea kutumia na kuiamini Benki ya CRDB katika huduma mbalimbali za kifedha.
“Tutaendelea kushika mkono Wilaya ya Mbogwe kwa sababu wananchi wameendelea kuiunga mkono Benki ya CRDB katika huduma zetu. Hivyo, nasi tutaendelea kurudisha sehemu ya mafanikio yetu kwa jamii,” amesema Wagana.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbogwe, Adestino Mwilinge, ameipongeza Benki ya CRDB kwa mchango huo, akisema hatua hiyo inaonyesha namna taasisi za kifedha zinavyoweza kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za kijamii, hususan sekta ya elimu.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kuiunga mkono Benki ya CRDB kwa kutumia huduma zake ili kuiwezesha kuendelea kutekeleza miradi yenye manufaa kwa jamii.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, Edwin Bayona Lusa, ameishukuru CRDB kwa msaada huo, akisema madawati yaliyotolewa yamepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya uhaba wa madawati katika shule hiyo.
Lusa amesema Serikali na Halmashauri zinaendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto za miundombinu ya elimu, akieleza kuwa tayari Serikali imepeleka zaidi ya Sh. milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo.


















Social Plugin