Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Baraza la Taifa la Watoto limeomba kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuwasilisha mapendekezo na changamoto zinazohusu ustawi, ulinzi na maendeleo ya watoto nchini.
Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watoto, Daniel Magembe, wakati wa uzinduzi wa Kanuni za Uanzishaji, Uendeshaji na Uratibu wa Mabaraza ya Watoto nchini, jijini Dodoma leo Septemba 11, 2026.
Magembe amesema kikao hicho kitatoa fursa kwa Baraza kuwasilisha kwa Rais masuala mbalimbali yanayowahusu watoto, yakiwemo maboresho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, hususan suala la umri wa kuolewa, pamoja na mahitaji ya kuboresha miundombinu inayotumika katika shughuli za watoto.
Amesema Baraza la Watoto kupitia Kamati Kuu limejadili mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuimarisha ulinzi na ustawi wa watoto, hivyo ni muhimu mapendekezo hayo yawasilishwe katika ngazi ya juu ya Serikali.
Kwa upande mwingine Magembe ameishukuru Serikali kwa hatua ya kuhakikisha Mabaraza ya Watoto yanatambulika kisheria.
Amesema kuwa utambuzi huo ni hatua muhimu katika kuimarisha nafasi ya mabaraza hayo katika kushughulikia na kuwasilisha masuala yanayowahusu watoto.
Hata hivyo, ameomba Serikali izingatie utengaji wa bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Mabaraza ya Watoto ili yaweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu inayotumika katika shughuli zinazohusu watoto ili iendane na mahitaji na wakati wa sasa.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju,ametumia nafasi hiyo kuwataka wadau wa maendeleo wanaojihusisha na masuala ya watoto kugawana maeneo ya kufanyia kazi badala ya kujikita katika eneo moja.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuimarisha uanzishwaji, uendeshaji na uratibu wa Mabaraza ya Watoto nchini.
Mpanju amesema Serikali inalenga kuhakikisha Mabaraza ya Watoto yanaanzishwa nchi nzima, hivyo ushirikiano na mgawanyo wa maeneo miongoni mwa wadau ni muhimu ili kufanikisha azma hiyo.
Amesema badala ya wadau wengi kufanya kazi katika eneo moja, ni muhimu kuwepo kwa ramani inayoonyesha nani anafanya nini na wapi, ili kuhakikisha huduma na shughuli za mabaraza hayo zinafanyika kwa ufanisi katika maeneo mbalimbali.
“Isiwe ni maneno ya jukwaani tu, tufanye mapping (ramani) ili kujua nani anafanya nini na wapi, kuhakikisha utekelezaji wa mabaraza unafanyika kwa ufanisi, kuanzia uanzishwaji, uendeshaji, ufuatiliaji na tathmini,” amesema.
Kwa mujibu wa Mpanju, lengo la Mabaraza ya Watoto ni kuwawezesha watoto kufahamu haki zao, kutambua na kuendeleza vipaji walivyonavyo, pamoja na kuwaandaa kwa maisha yao ya baadaye.
Aidha, Mpanju amewataka watendaji kuanzia ngazi ya Wizara kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuhakikisha mabaraza hayo yanaanzishwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema ushirikiano huo unapaswa kwenda sambamba na uwepo wa ramani ya utekelezaji itakayoonyesha namna wadau watakavyoratibu shughuli zao na kuhakikisha Mabaraza ya Watoto yanafanya kazi kwa ufanisi.
Naye Mratibu Taifa wa Jukwaa la Haki za Watoto, Ombeni Kimaro, amesema uwepo wa wadau mbalimbali wanaofanya kazi katika eneo la watoto unahitaji ushirikiano na uratibu mzuri ili kila mdau aweze kutekeleza majukumu yake kulingana na eneo na mahitaji yaliyopo.
Amesema hali hiyo itasaidia kupunguza mwingiliano wa shughuli na kuhakikisha maeneo yenye uhitaji mkubwa hayapitwi.
Amesema ni muhimu pia kuwepo kwa mawasiliano na ubadilishanaji wa taarifa miongoni mwa wadau ili kutambua shughuli zinazotekelezwa, maeneo yanayohitaji msaada na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Mabaraza ya Watoto.
Kimaro amesema Jukwaa la Haki za Watoto litaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine katika kuimarisha uratibu wa shughuli za watoto, ikiwemo ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji, ili kuhakikisha uwepo wa Mabaraza ya Watoto unaleta matokeo yanayokusudiwa kwa watoto nchini.

Social Plugin