
Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
Mkurugenzi wa Tupaze Sauti Foundation, Agness Suleiman Kahamba maarufu ‘Aggy Baby’, ametunukiwa tuzo ya Top Young Entrepreneur Awards 2026, katika kipengele cha kutambua mchango katika kuhamasisha ujasiriamali kwa jamii, hususan vijana na wanawake.
Tuzo hiyo imetolewa na Young Women Entrepreneurs Tanzania (YWE Tanzania) katika hafla iliyofanyika Jumamosi katika Ramada Hotel, Mbezi Beach, Dar es Salaam, ikiwakutanisha wajasiriamali na wadau mbalimbali wa maendeleo ya vijana na wanawake.
Kupitia tuzo hiyo, Agness ametambuliwa kwa mchango wake kupitia Tupaze Sauti Foundation katika kuhamasisha ujasiriamali na kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Akizungumza baada ya kutunukiwa tuzo hiyo, Agness amemshukuru Mungu kwa kutambuliwa kwa juhudi na mchango wake katika jamii, akisema tuzo hiyo ni faraja kubwa na chachu ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii.
“Namshukuru Mungu kwa kutunukiwa Tuzo ya Top Young Women Entrepreneur Awards 2026, iliyoandaliwa na YWE Tanzania. Tuzo hii ina maana kubwa sana kwangu. Ni faraja kuona juhudi, kazi na mchango wangu katika jamii ukitambuliwa ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.”
Agness amesema kutambuliwa huko kumempa nguvu zaidi ya kuendelea kujituma na kuweka juhudi katika kila anachokifanya, akilenga kuleta mabadiliko makubwa zaidi katika jamii.
“Kutambuliwa huku kunanipa nguvu zaidi ya kuendelea kupambana, kujituma na kuweka juhudi katika kila ninachokifanya ili niweze kuleta mabadiliko makubwa zaidi katika jamii.”
Amesema safari yake ya ujasiriamali imejengwa katika kujituma, kujitolea, uvumilivu na kutoa mchango katika maendeleo ya biashara na jamii.
“Utambuzi huu ni sehemu ya safari yangu ya ujasiriamali, kujitolea kwangu, uvumilivu na mchango wangu katika kukuza biashara na kuleta matokeo chanya katika jamii.”
Aidha, Agness amesema anajivunia kuwa sehemu ya kizazi kinachoshiriki katika kubadilisha sura ya biashara na ujasiriamali nchini Tanzania kwa kuibua thamani, kuleta matokeo chanya na kuchangia katika kujenga fursa mpya.
“Ninajivunia kuwa sehemu ya kizazi kinachobadilisha sura ya biashara na ujasiriamali nchini Tanzania. Tutaendelea kuunda thamani, kuleta matokeo yenye tija na kushiriki katika kujenga mustakabali wenye fursa zaidi.”
Tuzo hiyo imeongeza kutambua nafasi ya Tupaze Sauti Foundation katika kuhamasisha na kuchochea fursa za ujasiriamali, hasa kwa vijana na wanawake, ambao ni miongoni mwa makundi muhimu katika kujenga uchumi na maendeleo ya jamii.
Hafla ya Top Young Entrepreneur Awards 2026 imeandaliwa na Young Women Entrepreneurs Tanzania (YWE Tanzania) kwa lengo la kutambua na kuenzi mchango wa wajasiriamali na wadau mbalimbali wanaoshiriki katika kukuza ujasiriamali na maendeleo ya kiuchumi nchini.









Social Plugin