Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WMA DODOMA YAENDELEA KUTOA ELIMU NA KUKAGUA USAHIHI WA MASHINE ZA KUUZIA MAJI NA VIFAA VYA MAZOEZI (GYM)


Dodoma - WMA

Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Dodoma, Bw. Said Ibrahim, ameendelea na ziara ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara pamoja na kukagua vipimo vinavyotumika katika biashara ya kuuza maji ya kunywa mtaani na vile vinavyotumika kwenye kumbi za mazoezi (Gym) jijini Dodoma tarehe 11 Agosti, 2026.

Katika ziara hiyo, Bw. Said ametembelea maeneo mbalimbali yanayofanya biashara hizo, ikiwemo Makole, Makulu, Hazina, Wajenzi, Maili Mbili, Nkuhungu na Nyerere Square, kwa lengo la kujiridhisha kuwa vipimo vinavyotumika maeneo hayo vimehakikiwa na WMA.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Said amesema ukaguzi huo unaenda sambamba na utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kutumia vipimo sahihi na vinavyokidhi vigezo.

Amesema WMA imejiridhisha kuwa mashine za kuuza maji ya kunywa zilizotembelewa zinatoa vipimo sahihi kulingana na thamani ya fedha aliyotoa na ujazo wa maji ambao anauhitaji.

Aidha, katika kumbi za mazoezi, WMA imekagua vifaa mbalimbali vinavyohusiana na uzito na kujiridhisha kuwa vifaa hivyo viko sahihi, hatua inayolenga kuhakikisha usalama wa watu wanaotumia huduma hiyo ya mazoezi.

Bw. Said amesisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kuhakikisha vifaa vyao vinaendelea kuwa katika hali inayokidhi matakwa ya sheria, huku wananchi wakihimizwa kuwa makini na kuuliza pale wanapokuwa na mashaka kuhusu usahihi wa vipimo wanavyotumia.

Ziara hiyo ni sehemu ya jukumu la WMA za kuendelea kutoa elimu na kufanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha matumizi ya vipimo sahihi yanaimarika na wananchi wanapata huduma kwa haki na usalama.

“Kipimo Sahihi, Huduma Bora, Mteja Salama.”
WMA — Tunapima Usahihi, Tunalinda Haki.
Kwa mawasiliano na WMA piga namba 0800 110097

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com