Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKAGUZI WA MAFUTA WAIMARISHA UDHIBITI WA UBORA WAKATI WA UPAKUAJI



Serikali, kupitia Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), inasimamia upakuaji wa shehena za mafuta kutoka melini hadi kwenye maghala ya kuhifadhia mafuta, ili kuhakikisha usalama na uzingatiaji wa viwango vya ubora vinavyotakiwa.

Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane jijini Dodoma, Afisa Ubora wa Mafuta wa PBPA, Mhandisi Cyrill Makembe, amesema mchakato wa upakuaji wa mafuta unahusisha hatua mbalimbali zinazohitaji uangalizi wa karibu wa wataalamu.

Amesema Wakaguzi wa Mafuta (Petroleum Inspectors) hufuatilia mchakato mzima wa upakuaji ili kuhakikisha taratibu zilizowekwa zinafuatwa na ubora wa mafuta unalindwa katika kila hatua.

“Mafuta yanapowasili nchini, Wakaguzi wa Mafuta hufuatilia hatua mbalimbali za upakuaji ili kuhakikisha yanakidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa,” amesema Mhandisi Makembe.

Ameeleza kuwa ufuatiliaji huo huanza mafuta yakiwa ndani ya meli na kuendelea wakati wa upakuaji na usafirishaji kupitia miundombinu maalumu, hadi yanapofikishwa kwenye maghala yaliyokusudiwa kwa ajili ya kuhifadhiwa.

Kwa mujibu wa Mhandisi Makembe, Baada ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuidhinisha ubora wa bidhaa za mafuta kabla Meli haijaanza zoezi la Upakuaji ,Wakaguzi wa Mafuta wanajukumu la kuhakikisha kuwa taratibu za usalama na masharti ya upakuaji yanazingatiwa katika mchakato mzima wa upakuaji wa mafuta hayo. Hatua hiyo inalenga kulinda ubora wa mafuta na kuhakikisha shughuli za upakuaji zinafanyika kwa usalama.

Aidha, ukaguzi huo unalenga kubaini mapema changamoto zozote zinazoweza kuathiri ubora wa mafuta wakati wa upakuaji, usafirishaji au uhifadhi. Hatua hiyo husaidia kuhakikisha mafuta yanayopokelewa yanaendelea kuwa katika hali inayokubalika na TBS hadi yanapofikishwa kwenye maghala husika.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com