Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Serikali imeeleza kuridhishwa na mchango wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) katika kuimarisha afya ya mimea, kudhibiti visumbufu vya mazao na kuwajengea wakulima uwezo wa kutumia viuatilifu kwa usalama, hatua zinazochochea ongezeko la uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 1, 2026 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, baada ya kutembelea banda la TPHPA katika Maonesho ya 33 ya Siku ya Wakulima (Nanenane 2026) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, ambapo aliipongeza mamlaka hiyo kwa huduma zake zinazowanufaisha wakulima na kuitaka iendelee kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Katika ziara hiyo, Dkt. Nchemba aliambatana na Waziri wa Kilimo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi pamoja na mawaziri wengine wa Serikali, na kupokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph Ndunguru, ambaye alimweleza mafanikio ya mamlaka hiyo katika kuboresha afya ya mimea nchini.
Prof. Ndunguru amesema TPHPA imeongeza juhudi katika kudhibiti baa la panzi, kutoa elimu ya matumizi salama ya viuatilifu na kuhakikisha afya ya mimea inalindwa ili kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima.
Dkt. Nchemba amesema utendaji wa TPHPA unaendana na kaulimbiu ya Maonesho ya Nanenane 2026 isemayo, "Tambua Soko; Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050," na kusisitiza mamlaka hiyo iendelee kuboresha huduma zake ili kulinda mazao, kuongeza uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Social Plugin