Na Sheila Ahmadi, Dodoma

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imewataka wananchi kutumia fursa ya Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima maarufu kama Nanenane kupata elimu kuhusu huduma mbalimbali za bima, ikiwemo bima ya kilimo.

Akizungumza katika maonesho hayo yanayofanyika jijini Dodoma, Afisa anayehusika na Mawasiliano kwa Umma kutoka TIRA, Anna Massau, amesema mamlaka hiyo imeshiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima katika kujikinga na changamoto na hasara mbalimbali.

Amesema TIRA imeweka maafisa katika banda lake ambao wanatoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya bima, huku wananchi wakipata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu huduma hizo.

“Tunawakaribisha wananchi wa Dodoma pamoja na Watanzania wote kwa ujumla kutembelea banda letu ili kupata elimu kuhusu bima, ikiwemo bima ya kilimo,” amesema Massau.

pamoja na kutoa elimu, TIRA ina majukumu mbalimbali ikiwemo kusajili na kutoa leseni kwa watoa huduma za bima, pamoja na kuandaa kanuni na miongozo inayotumika katika sekta hiyo.

Aidha, amesema mamlaka hiyo ina jukumu la kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya wananchi yanayohusu masuala ya bima, hivyo wananchi wenye changamoto wanakaribishwa kufika katika banda hilo kwa ajili ya kupata msaada.

Katika hatua nyingine Massau amesema katika maonesho hayo TIRA pia imewashirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya bima, wakiwemo kampuni za bima pamoja na Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima, ili wananchi waweze kupata huduma na majibu ya maswali yao kwa urahisi.

“Tunawakaribisha sana wananchi wote kutembelea banda letu. Tupo na maafisa wengi ambao watawapatia elimu kuhusu masuala yote ya bima, na kama una changamoto au malalamiko yanayohusu bima, tutakusikiliza na kukusaidia,”

ushiriki wa TIRA katika Nanenane ni sehemu ya jitihada za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu bima na kuwahamasisha kutumia huduma hizo katika kulinda shughuli zao za kiuchumi, hususan sekta ya kilimo.