Na Atley Kuni, WAF-MBEYA
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt. Elizabeth Nyema, amewataka wananchi kutumia tiba asili kwa uangalifu na kuhakikisha wanapata huduma kutoka kwa wataalamu wanaotambulika, akisisitiza usalama wa mgonjwa, ubora wa dawa na ushahidi wa kisayansi vinapaswa kuwa msingi wa matumizi na maendeleo ya tiba hiyo.
Dkt. Nyema ametoa kauli hiyo Agosti 27, 2026 wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika yanayofanyika nchini kuanzia Agosti 25 hadi 31, 2026, huku kilele cha maadhimisho hayo kikitarajiwa kufanyika Agosti 31 katika Viwanja vya Uhindini, jijini Mbeya.
Amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu, “Juhudi katika Utafiti za Tiba Asili katika kuelekea Huduma za Afya kwa Wote,” inalenga kuwakumbusha wananchi na wadau kuwa maendeleo ya tiba asili yanahitaji utafiti, uthibitishaji wa kisayansi na matumizi salama.
"Tiba asili ni sehemu ya rasilimali za afya, maarifa ya jamii na urithi wa Watanzania, hivyo ni muhimu kuendelezwa kwa namna inayomlinda mwananchi na wakati huo huo kutoa fursa ya kubaini tiba zenye manufaa halisi kwa afya ya jamii", amesema Dkt. Nyema.
Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika huadhimishwa, ikiwa ni kumbukumbu ya Azimio Na. AFR/RC50/R3 lililopitishwa na Mawaziri wa Afya wa nchi za Kanda ya Afrika kwenye kikao cha 50 cha Kamati ya WHO kwa Kanda ya Afrika kilichofanyika Burkina Faso mwaka 2000. Siku hiyo ilianza kuadhimishwa mwaka 2003.
Kwa mujibu wa Dkt. Nyema, Tanzania imeendelea kuweka mifumo ya kuhakikisha sekta ya tiba asili inakuwa na utaratibu unaolinda maslahi ya wananchi kwa kuwa na Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007, Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala, Sura ya 244, pamoja na Mpango Mkakati wa Tano wa Sekta ya Afya wa 2021–2026 kwa kusimamia masuala ya usajili, udhibiti wa bidhaa, maadili ya kitaaluma, utafiti na ushirikiano kati ya watoa tiba asili na wataalamu wa tiba za kisasa.
Maadhimisho hayo yanaendana pia na Mkakati wa Shirika la Afya Duniani wa Tiba Asili wa 2025–2034, uliopitishwa katika Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Afya Duniani mwezi Mei 2025, ambapo Tanzania imeendelea kuonyesha dhamira ya kuimarisha ujumuishaji unaofaa wa tiba asili, hususan katika huduma za afya ya msingi" amesema Dkt. Nyema.
Dkt. Nyema amehitimisha kwa kuwaalika wananchi na wadau kushiriki kikamilifu katika shughuli za Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika hadi kilele chake Agosti 31, 2026, katika Viwanja vya Uhindini, Mbeya. Amesema maadhimisho hayo ni fursa kwa wananchi kupata elimu, kuuliza maswali na kuelewa haki zao kuhusu huduma na bidhaa za tiba asili ya Mwafrika.



Social Plugin