Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
MOROGORO: Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni linalotarajiwa kufanyika mkoani Morogoro kuanzia Agosti 25 hadi 29, 2026, limeelezwa kuwa ni nyenzo muhimu ya kufungamanisha utamaduni na uchumi, huku likilenga kuhifadhi, kuendeleza na kutangaza urithi wa Watanzania.
Tamasha hilo pia linalenga kuimarisha utambulisho wa Taifa na historia yake kwa vizazi vya sasa na vijavyo, pamoja na kutoa fursa kwa wananchi kutumia utamaduni, sanaa na ubunifu kama chanzo cha ajira na kipato.
Akizungumza Agosti 23, 2026 mbele ya waandishi wa habari katika Kambi ya Wapigania Uhuru Mazimbu, Morogoro, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kufanyika kwa tamasha hilo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kulinda na kuendeleza utamaduni wa Mtanzania.
Amesema utamaduni unapaswa kutumika kujenga maadili, kuimarisha utaifa na mshikamano, kukuza uchumi bunifu, kuongeza fursa za ajira na biashara, pamoja na kuitangaza Tanzania kupitia utalii wa kiutamaduni.
“Tamasha la Utamaduni limeandaliwa kwa mtazamo mpana unaounganisha utamaduni na uchumi kwa lengo la kuhakikisha sanaa na urithi wa Taifa vinakuwa sehemu ya kuchochea maendeleo na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi. Tamasha hilo siyo la kuangalia tu bali kushiriki, kujifunza, kubuni, kufanya biashara na kujenga uhusiano,” amesema Msigwa.
Akizungumzia kauli mbiu ya tamasha hilo isemayo “Utamaduni Wetu, Nguzo ya Maadili, Uchumi Jumuishi na Utaifa, Karibu AFCON 2027,” Msigwa amesema inalenga kusisitiza umuhimu wa maadili, uchumi jumuishi na utaifa.
Amesema pia kauli hiyo inaendana na maandalizi ya Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda kuwa wenyeji wa michuano ya AFCON 2027, hivyo tamasha hilo litatoa nafasi ya kuunganisha utamaduni na maandalizi ya tukio hilo kubwa la kimataifa.
Kwa mujibu wa Msigwa, tamasha hilo linatarajiwa kuwakutanisha washiriki kutoka mikoa 26, vikundi vya utamaduni 28, wasanii 30, wajasiriamali 70, vijana takribani 5,000 na taasisi za washirika 70, huku wananchi na wageni wakitarajiwa kufikia 150,000.
Aidha, tamasha hilo litakuwa na shughuli mbalimbali zipatazo 120, zikiwemo maonesho ya vyakula vya asili 100, maonesho ya bidhaa za utamaduni na ubunifu zaidi ya 150, pamoja na fursa za biashara zinazokadiriwa kufikia 70.
Kwa ujumla, Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni linatarajiwa kuwa jukwaa la kuunganisha urithi wa Tanzania na fursa za kiuchumi, huku likitoa nafasi kwa wananchi, wasanii, wajasiriamali na vijana kushiriki katika kuutangaza na kuutumia utamaduni kama kichocheo cha maendeleo.

Social Plugin