Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAFITI KUWA CHACHU YA USAFIRI BORA, UCHUMI IMARA – PROFESA MBARAWA



Na Sheila Ahmadi, Dar es salaam.

Serikali imetoa wito kwa watafiti kutumia tafiti zao kutengeneza suluhisho zitakazosaidia kupunguza gharama za usafirishaji, kuongeza ufanisi wa bandari na reli, pamoja na kuimarisha usalama wa usafiri nchini.

Ambapo Imesema mfumo bora wa usafiri ni miongoni mwa nguzo muhimu za kukuza uchumi wa Tanzania, kuongeza biashara na kuimarisha uhusiano wa kibiashara na nchi za ukanda wa Afrika.

Akizungumza Jijini Dar es salaam kwenye mkutano wa watafiti na wadau wa sekta ya usafiri Waziri Wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema Tanzania inapotekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo, mfumo wa usafiri unapaswa kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi, badala ya kusubiri maendeleo ya sekta nyingine.

Vilevile tafiti zinapaswa kusaidia kubaini namna ya kupunguza gharama za usafirishaji, kuboresha ufanisi wa bandari na reli, kuongeza usalama wa usafiri, kutumia teknolojia mpya na kujenga miundombinu inayoweza kuhimili changamoto mbalimbali, ikiwemo athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Utafiti unatakiwa utusaidie kupata majibu ya matatizo halisi, kupunguza gharama za usafirishaji, kuboresha ufanisi wa bandari pamoja na reli zetu na kuongeza usalama wa usafiri hapa nchini,” amesema Profesa Mbarawa

Nitoe wito kwa watafiti kutumia mkutano huo kuwasilisha mapendekezo yenye mwelekeo wa kutatua changamoto zilizopo, akisisitiza kuwa mafanikio ya mkutano hayapaswi kupimwa kwa idadi ya washiriki au mada zitakazowasilishwa pekee.

Tanzania inahitaji kujenga mfumo wa usafiri ulio salama, unaounganisha maeneo mbalimbali, wenye ushindani na unaoweza kusafirisha watu na mizigo kwa ufanisi na gharama nafuu.

Kupitia Mkutano huu watafiti na wadau wa sekta ya usafiri waendelee kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatumika katika kuboresha sera, mipango na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dkt. Prosper Mgaya, amesema kongamano la nne la usafirishaji limeendelea kupanua wigo wake kimataifa, huku idadi ya washiriki kutoka nje ya Tanzania ikiongezeka kwa kasi.

Dkt. Mgaya amesema washiriki wa kimataifa wameongezeka kutoka wawili katika kongamano la kwanza lililofanyika mwaka 2023 hadi kufikia 16 mwaka huu, jambo alilosema linaonesha kuongezeka kwa hadhi na mvuto wa kongamano hilo katika ngazi ya kimataifa.

“Ongezeko hili ni ishara kuwa kongamano hili sasa limejenga hadhi ya kimataifa, huku baadhi ya wataalamu wakitoka Japan na Uingereza kushiriki moja kwa moja katika kongamano hilo,” alisema Dkt Mgaya.

Amesema ushiriki wa wataalamu hao unatoa fursa kwa Tanzania kujifunza uzoefu na maarifa mapya katika sekta ya usafirishaji, pamoja na kujadili namna ya kutumia tafiti na teknolojia kuboresha huduma za usafiri.

Dkt. Mgaya pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha muunganiko wa aina mbalimbali za usafiri, ikiwemo reli, anga na majini, ili kuongeza ufanisi katika usafirishaji wa abiria na mizigo.










Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com