
Na Elizabeth Cosmas - Shinyanga
SHYCOM Mapendo Sports Promotion, waandaaji wa Shycom Alumni Half Marathon, leo Agosti 15, 2026 wamezindua rasmi msimu wa pili wa mbio hizo za hisani, sambamba na kutambulisha vifaa vitakavyotumika katika mashindano hayo, ikiwemo jezi, medali na vifaa vingine.
Mbio hizo ambazo zinatarajiwa kufanyika Septemba 26, 2026, zinalenga kuhamasisha wananchi wa Shinyanga kushiriki katika michezo kama sehemu ya kuimarisha afya, huku fedha zitakazopatikana zikilenga kusaidia kuboresha miundombinu katika Chuo cha Shycom.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Josta Dominick, Katibu wa Kamati ya Maandalizi, amesema kurejea kwa mbio hizo katika msimu wa pili kumelenga kuendeleza miradi ya maendeleo ndani ya chuo hicho, ikiwemo kuboresha zahanati pamoja na kujenga na kuboresha njia za kutembelea ndani ya chuo.
Josta amesema katika msimu wa kwanza wa Shycom Alumni Marathon uliofanyika mwaka 2024, waandaaji walifanikiwa kuboresha mabweni mawili, na kwamba msimu huu wamejipanga kuweka vitanda katika mabweni hayo pamoja na kuboresha njia za kutembelea.
“Katika msimu wa kwanza wa Shycom Marathon uliofanyika mwaka 2024, tulifanikiwa kuboresha mabweni mawili. Katika msimu huu tunahitaji kuweka vitanda ndani ya mabweni tuliyokarabati, lakini pia tunahitaji kuboresha njia za kutembelea ili wanafunzi wanapoingia bwenini wasiingie kwenye matope, hasa katika nyakati za mvua.”
Aidha, Josta amesema kamati imeamua kuendesha mbio hizo kama mbio za hisani kwa kuamini kuwa kukimbia ni sehemu ya kuimarisha afya, huku pia zikitumika kuwaunganisha wanafunzi, wahitimu na wadau mbalimbali wa Shycom katika kuchangia maendeleo ya chuo.
Amesema mbio hizo pia ni sehemu ya kutoa shukrani kwa chuo hicho kwa mchango wake kwa jamii, huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki.
Kwa upande wake, Omary Mwenda, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga, amewapongeza waandaaji wa Shycom Alumni Half Marathon kwa kurejesha mbio hizo kwa msimu wa pili, akisema zimekuwa chachu ya maendeleo katika kuboresha miundombinu ya chuo.
Mwenda amesema jitihada hizo zinaunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu na kuongeza ustawi wa wananchi.
“Niwashukuru sana waandaaji wa mbio hizi za Shycom Alumni Marathon kwa kuona thamani ya kile kilichofanyika msimu wa kwanza mwaka 2024 na kuweza kuleta msimu huu wa pili, ukiwa na lengo la kujali afya zetu kupitia kukimbia, lakini pia kuendeleza jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ndani ya mkoa wetu”
Amesema kupitia mbio hizo, miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Shinyanga inaendelea kuimarika, huku akiwataka wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono mipango inayolenga kuleta maendeleo katika jamii.
Naye Samwel Anthony, Mwenyekiti wa Chama cha Wanariadha Mkoa wa Shinyanga, amesema chama hicho kimejipanga kushiriki kikamilifu katika msimu wa pili wa mbio hizo, kama ilivyokuwa katika msimu wa kwanza.
Samwel amewataka wadau wa michezo pamoja na wananchi wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo, akisema ni sehemu ya kuchangia juhudi za kuboresha miundombinu ya Chuo cha Shycom na wakati huo huo kuimarisha afya za wananchi.
“Sisi kama Chama cha Wanariadha tumejipanga kwa ukubwa kuhakikisha tunashiriki kikamilifu katika mbio hizo, huku tukiendelea kushika mkono jitihada za kuboresha miundombinu inayofanyika ndani ya Chuo cha Shycom.”
Shycom Alumni Half Marathon msimu wa pili inatarajiwa kufanyika Septemba 26, 2026, ikiwa ni mbio za hisani zinazolenga kuunganisha michezo, afya na maendeleo ya jamii kupitia uchangiaji wa miradi ya maendeleo ndani ya Chuo cha Shycom.


















Social Plugin