Na Dotto Kwilasa, Dodoma
SERIKALI imesema zama za Tanzania kuuza mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi yakiwa ghafi zinapaswa kubadilika, ikisisitiza umuhimu wa kuimarisha viwanda vya kuongeza thamani ili wazalishaji wanufaike zaidi na kuongeza mchango wa sekta hizo katika uchumi wa taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo katika Maonyesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dk. John Samuel Malecela, Dodoma, ambako Wizara ya Viwanda na Biashara imeweka mkazo katika kuwaunganisha wakulima, wafugaji na wavuvi na fursa za viwanda, biashara na masoko.
Akizungumza katika maonyesho hayo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Denis Londo amesema kilimo, mifugo na uvuvi haviwezi kutenganishwa na sekta ya viwanda na biashara kwa kuwa mazao yanayotokana na sekta hizo ni bidhaa kwa ajili ya masoko na wakati huo huo ni malighafi muhimu kwa viwanda.
“Maonyesho haya ni ya kilimo, mifugo na uvuvi. Kimsingi hizo zote ni bidhaa. Sisi tunaingia hapa kama Wizara ya Viwanda na Biashara kwa maana hizo zote ni biashara na zote ni mali ghafi kwa ajili ya viwanda vyetu,” amesema.
Amesema Serikali inalenga kujenga mnyororo wa thamani utakaoifanya Tanzania kunufaika zaidi na uzalishaji wake kwa kuhakikisha mazao yanabadilishwa kuwa bidhaa zenye thamani kubwa kabla ya kufikishwa katika masoko.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga kujenga uchumi shindani unaotegemea uzalishaji, viwanda na bidhaa zenye uwezo wa kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
WAKULIMA KUPUNGUZIWA GHARAMA
Akizungumzia namna Serikali inavyolenga kumwezesha Mtanzania kuongeza tija katika uzalishaji, Naibu Waziri alisema moja ya vipaumbele ni kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.
Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wazalishaji hao, ikiwemo kuboresha miundombinu inayowaunganisha na masoko pamoja na viwanda.
“Tunachowaahidi ni kuhakikisha tunamtengenezea mazingira rafiki Mtanzania, awe mkulima, awe mvuvi au awe mfugaji. Kwanza katika kuhakikisha kwamba tunampunguzia gharama za uzalishaji,” amesema.
Ameeleza kuwa kupungua kwa gharama za uzalishaji kutampa nafasi Mtanzania kuongeza faida, kuzalisha kwa tija na kubaki na kipato cha kutosha baada ya kuuza mazao yake.
Amesema uwekezaji katika barabara, madaraja na vivuko ni sehemu ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka maeneo ya uzalishaji kwenda kwenye masoko na viwandani.
UMEME, MAWASILIANO KUONGEZA TIJA
Naibu Waziri amesema upatikanaji wa umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pia ni muhimu katika kuchochea shughuli za kuongeza thamani ya mazao katika maeneo ya uzalishaji.
Amesema umeme unawawezesha wananchi kuanzisha shughuli za uzalishaji na uchakataji wa mazao karibu na maeneo wanayozalisha, badala ya kutegemea kuuza mazao ghafi.
Aidha, Serikali imeendelea kuboresha mawasiliano kwa kujenga minara katika vijiji na vitongoji, hatua inayolenga kuwawezesha wazalishaji kupata taarifa kuhusu masoko na mwenendo wa biashara.
“Tunataka Mtanzania awe na uhakika wa kujua soko linaendaje na kupata taarifa za uhakika ili afanye maamuzi ya uhakika ambayo yatamhakikishia tija katika shughuli zake za uzalishaji,” amesema.
BRELA, TBS, SIDO NA FCC KUWA KARIBU NA WANANCHI
Katika Maonyesho ya Nanenane, Wizara ya Viwanda na Biashara imewakutanisha wananchi na taasisi zake mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu na huduma zinazohusu biashara, viwanda na ujasiriamali.
Taasisi hizo ni pamoja na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Tume ya Ushindani (FCC) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).
BRELA inatoa huduma za usajili wa majina ya biashara na makampuni pamoja na elimu kwa wananchi wanaotaka kuanzisha shughuli za biashara, huku TBS, FCC na SIDO zikiendelea kutoa huduma na elimu kulingana na majukumu yao.
Kwa upande wa SIDO, wananchi na wajasiriamali wanapata elimu kuhusu namna ya kuendeleza viwanda vidogo, kuongeza thamani ya bidhaa na kuboresha uzalishaji.
Wizara imesema uwepo wa taasisi hizo katika Nanenane unalenga kumrahisishia Mtanzania kupata huduma na taarifa mbalimbali sehemu moja, huku akipata fursa ya kujifunza namna ya kushiriki kikamilifu katika biashara na uzalishaji.
LENGO NI TANZANIA YA BIDHAA, SI MALIGHAFI
Akisisitiza umuhimu wa kuongeza thamani, Serikali imesema Tanzania haiwezi kutegemea kuuza malighafi pekee wakati ina uwezo wa kuzalisha bidhaa zinazoweza kuuzwa kwa thamani kubwa zaidi.
Kwa mtazamo huo, mkulima, mfugaji na mvuvi wanaonekana kuwa sehemu muhimu ya mnyororo wa thamani unaounganisha uzalishaji, viwanda, biashara na masoko.
Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira wezeshi, kutoa elimu na kuimarisha taasisi zinazohusika na biashara na viwanda ili kuwawezesha wananchi kutumia fursa zilizopo kuongeza thamani ya bidhaa zao.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha ongezeko la uzalishaji linaenda sambamba na ongezeko la thamani ya mazao, kipato cha wazalishaji, ajira na mapato ya taifa, katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi unaotegemea zaidi uzalishaji na viwanda.

Social Plugin