Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAIMARISHA ULINZI WA WATOTO DHIDI YA UKATILI MTANDAONI



Na Jackline Minja, Dodoma

Serikali imeendelea kuimarisha hatua za kulinda watoto dhidi ya ukatili, unyanyasaji, unyonyaji na madhara mengine yanayotokana na matumizi ya mitandao ya kijamii.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati akijibu swali la Mhe. Lucy Simirya Kombani (Viti Maalum), kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya ukatili mtandaoni.

Naibu Waziri Mahundi amesema miongoni mwa hatua zinazotekelezwa ni Kampeni ya Kitaifa ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto Mtandaoni, ambayo imefanyika katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara kwa lengo la kutoa elimu kwa watoto, wazazi, walezi na jamii kuhusu matumizi salama na yanayolinda haki za watoto mtandaoni.

“Jumla ya watoto 1,811,212 wamefikiwa na elimu kuhusu usalama wa mtoto mtandaoni aidha, kampeni hiyo imehusisha wawezeshaji 516 kutoka ngazi za mikoa, wakiwemo Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa Elimu, Dawati la Polisi la Jinsia na Watoto pamoja na SMAUJATA” amesema Mahundi.

Ameongeza kwamba Serikali imeunda Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu Ulinzi na Usalama wa Mtoto Mtandaoni, yenye jukumu la kutoa ushauri wa kitaalamu na kusaidia Serikali kuweka mikakati na afua madhubuti za kuzuia na kukabiliana na vitendo vya ukatili pamoja na madhara yanayoweza kuwakabili watoto wanapotumia mifumo ya kidijitali.

Vilevile, Serikali imefanya maboresho ya Sheria ya Mtoto Sura ya 13, ambapo kifungu kinachohusiana na makosa ya kimtandao kimefanyiwa marekebisho ili kuweka masharti yanayohusiana na makosa ya unyanyasaji na utumikishaji wa kingono kwa watoto kwa kutumia nyenzo za TEHAMA, hatua inayolenga kuwalinda watoto dhidi ya uhalifu wa kingono mtandaoni.

Aidha, Serikali imeeleza kuwa matumizi yasiyo salama ya mitandao yanaweza kusababisha madhara mbalimbali kwa watoto, ikiwemo kuathirika kisaikolojia kutokana na kuangalia maudhui yasiyoendana na umri wao, uraibu unaotokana na kutumia muda mwingi mtandaoni pamoja na mmomonyoko wa maadili unaoweza kusababishwa na kuiga mila na desturi za mataifa mengine hivyo wazazi na walezi wahakikishe wanafuatilia mienendo ya watoto wao pindi wanapowanunulia vifaa hivyo vya teknolojia.

Katika kuhakikisha ulinzi wa mtoto unaanzia ndani ya familia, Serikali imewataka wazazi na walezi kujenga mahusiano mazuri na watoto kuhusu matumizi ya TEHAMA, kuwa karibu nao wanapotumia mitandao na kufuatilia shughuli zao mtandaoni, ikiwemo kutumia mifumo ya Parental Control.

Wazazi na walezi wanapaswa kufundisha watoto kufikiria kwa makini kabla ya kutuma picha, video au ujumbe wowote mtandaoni, kwa kuwa taarifa iliyowekwa mtandaoni inaweza kuwa vigumu kuiondoa kabisa, Pia niwamehimize watoto kuzungumza na watu wanaowaamini pindi wanapoona dalili au kufanyiwa vitendo vya ukatili mtandaoni.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com