Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUPITIA MFUMO WA BIASHARA NA UCHIMBAJI WA MADINI YA TANZANITE



▪️Rais Samia Apongezwa Kwa Kuelekeza Asilimia 10 ya mapato ya Sekta ya Madini kwenye utafiti wa kina wa madini

▪️Waziri Mavunde aelekeza nguvu ya Utafiti madini wa kina Mirerani

▪️Atoa wiki 2 kwa wazalishaji wakubwa kuja na mpango wa kuongeza uzalishaji

▪️Kofia Ngumu Zenye Kamera Maalum Kuanza Kutumika Kufuatilia Uchimbaji Chini ya Migodi

▪️Wizara za Madini na Wizara ya Nishati Zaja na Mkakati wa Umeme Maeneo ya Shughuli za Madini

▪️Serikali Yafungua Njia ya Mitaji Kupitia Dhamana za Mikopo

📍 Mirerani, Manyara. 

Serikali kupitia Wizara ya Madini imeanza kuchukua hatua za kuboresha mfumo wa biashara na uchimbaji wa madini ya Tanzanite nchini, kwa kufikia maamuzi yaliyotokana na taarifa za Tume na Kamati zilizoundwa kuchunguza changamoto za sekta hiyo, kwa ajili ya kuboresha mazingira ya biashara, kuimarisha usimamizi na kuongeza uzalishaji wa madini hayo adimu duniani sambamba na kuongeza thamani. 

Mhe. Mavunde ametoa maelekezo hayo leo, Agosti 24, 2026, wakati wa ziara ya kukagua shughuli za uchimbaji na biashara ya Tanzanite Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, ambapo ametembelea migodi inayomilikiwa na Franone Mining & Gems Co. Ltd. Na Chusa Mining Limited,soko dogo la madini,eneo la uthaminishaji na jengo la biashara ya madini ya Tanzanite.

Aidha Waziri  Mavunde, ametoa wiki mbili kwa wachimbaji wa kati wa madini ya Tanzanite Mirerani kuwasilisha taarifa ya hatua wanazochukua katika kutumia teknolojia za kisasa za utafiti, akisisitiza kuwa sayansi na teknolojia ni muhimu katika kubaini mashapo yaliyopo na kuongeza uzalishaji wa madini hayo adimu duniani sambamba na kuacha uchimbaji wa kubahatisha kwa kukosa taarifa sahihi.

“Wekezeni kwenye teknolojia ya kisasa ya utafiti, wekezeni kwenye sayansi ili kubaini mashapo yaliyopo. Ndani ya wiki mbili kuanzia nataka kupata taarifa ya juhudi zenu za uwekezaji katika teknolojia ya kisasa ya utafiti,” amesema Mhe. Mavunde.

Aidha, Waziri Mavunde amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maelekezo ya kutenga asilimia 10 ya mapato yatokanayo na Sekta ya Madini kwa ajili ya utafiti, akisema uamuzi huo utaongeza kasi ya utafiti wa kina wa rasilimali za madini nchini.

Amesema Mirerani na Mkoa wa Manyara ni miongoni mwa maeneo ya kipaumbele katika mpango huo wa utafiti, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa rasilimali zilizopo na kuwezesha shughuli za uchimbaji kufanyika kwa ufanisi zaidi.

Akizungumzia upatikanaji wa mitaji, Mhe. Mavunde amesema wachimbaji wanaweza kunufaika na mikopo nafuu kupitia taasisi za fedha, huku Serikali ikiendelea kuimarisha mifumo ya dhamana za mikopo.

Amesema Shirika la Mfuko wa Dhamana za Mikopo (Credit Guarantee Scheme Corporation) kupitia Benki Kuu ya Tanzania tayari umeundwa na kusajiliwa, na unatarajiwa kusaidia wachimbaji kupata mitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde, ametangaza kuanza kutumika kwa kofia ngumu yenye kamera katika migodi ya Mirerani, teknolojia itakayowezesha ufuatiliaji wa shughuli za uchimbaji hata chini ya mgodi kwa kuanza na Mgodi wa Franone Mining & Gems Co. Ltd na kuelekeza migodi mingine kutumia teknolojia hiyo ili kuongeza ufanisi katika usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za uchimbaji.

Kuhusu changamoto ya nishati ya umeme, Mhe. Mavunde amesema Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati zimeweka mkakati wa pamoja wa kuhakikisha upatikanaji wa nishati unaendana na mahitaji ya Sekta ya Madini, ili shughuli za uchimbaji na shughuli zingine zinazoambatana na Sekta ya Madini ziendelee bila vikwazo.

Aidha, Mhe. Mavunde amewapongeza wadau wa Mirerani kwa kushiriki minada ya madini pamoja na kuchangia huduma za kijamii, ikiwemo ujenzi wa zahanati, akisisitiza umuhimu wa Sekta ya Madini kuendelea kuwa na manufaa kwa jamii.

Aidha, amepiga marufuku wafanyabiashara wa madini (dealers) kutumia wageni kufanya biashara kinyume na utaratibu, akionya kuwa Serikali itachukua hatua kali dhidi ya watakaokiuka sheria.

 Sambamba na hilo, amemuelekeza Afisa Madini Mkazi wa Mirerani kukutana na kampuni za uchimbaji na wadau wengine ili kuboresha mazingira ya kazi kwa wanaapolo, huku Ofisi hiyo ikitakiwa kukaa na wadau wote kuangalia namna bora ya kuboresha mazingira ya biashara katika soko lililopo ndani ya migodi.

Waziri Mavunde pia ameiagiza Kituo cha Jemolojia Tanzania  (TGC) kutembelea wanawake wanaojihusisha na shughuli za magonga katika eneo la Mirerani na kutathmini namna ya kuwawezesha zaidi. 

Aidha, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kuangalia uwezekano wa kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa wananchi kwa kuzingatia shughuli za uchimbaji wa madini ambazo ndizo shughuli kuu za kiuchumi katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Simanjiro na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. James Kinyasi Ole Millya, amemshukuru Waziri Mavunde kwa kutembelea Mirerani na kuchukua hatua za kushughulikia changamoto zinazowakabili wachimbaji na wananchi wa eneo hilo.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer, ameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, akisema hatua zinazochukuliwa zinaendelea kuimarisha shughuli za madini na maendeleo ya wananchi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mkurugenzi wa Franone Mining, Onesmo Mbise, na Mkurugenzi wa Chusa Mining, Joseph Mwakipesile, wametoa ahadi mbele ya Waziri Mavunde kutekeleza maelekezo hayo kwa kufanya utafiti wa kisasa wa mashapo ya Tanzanite na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji ndani ya muda uliowekwa.











Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com