Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RUWASA KWA KUSHIRIKIANA NA WADAU WAJA NA MKAKATI WA KUSHUGHULIKIA SUALA LA USAFI WA MAZINGIRA VIJIJINI


Morogoro

Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Sekta ya Maji, Afya na Usafi wa Mazingira, umeanza rasmi mchakato wa kuandaa Mkakati wa RUWASA wa Menejimenti ya Tope Kinyesi (Faecal Sludge Management Strategy), unaolenga kuweka mfumo madhubuti, salama na endelevu wa menejimenti ya tope kinyesi katika maeneo ya vijijini.

Akifungua Kikao Kazi cha National Task Force kinachofanyika mjini Morogoro, Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Eng. Wolta S. Kirita, amesema maandalizi ya Mkakati huo ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za usafi wa mazingira vijijini na kupunguza athari za kiafya na kimazingira zinazoweza kusababishwa na menejimenti isiyo salama ya tope kinyesi.

Eng. Kirita amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau katika kuhakikisha Mkakati utakaoandaliwa unazingatia mazingira halisi ya vijijini, unaweka bayana majukumu ya wadau mbalimbali na, muhimu zaidi, unatekelezeka na kuwa endelevu.

“Pamoja na jukumu letu kubwa la kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma endelevu za maji, RUWASA pia ina wajibu katika masuala ya usafi wa mazingira. Tupo tayari kushirikiana na wadau wote kuhakikisha tunakuwa na mfumo bora na endelevu wa menejimenti ya tope kinyesi katika maeneo ya vijijini,” amesema Eng. Kirita.

Awali, akimkaribisha Mkurugenzi Mkuu, Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Eng. Mariam Majala, amesema menejimenti salama ya tope kinyesi bado ni changamoto inayohitaji juhudi za pamoja za kitaalamu na kitaasisi.

Eng. Majala amesema maandalizi ya Mkakati huo yatawezesha kuweka mwelekeo wa pamoja kuhusu namna bora ya kukusanya, kusafirisha, kutibu na kutupa au kutumia tena tope kinyesi kwa njia salama, sambamba na kuweka mpango na mwongozo wa utekelezaji unaozingatia mazingira na mahitaji ya maeneo ya vijijini.

Kikao Kazi hicho cha siku nne kinawaleta pamoja wajumbe wa National Task Force kutoka RUWASA, Wizara na Taasisi za Serikali, Vyuo Vikuu, Wadau wa Maendeleo pamoja na wataalamu wenye uzoefu katika Sekta ya Maji na Usafi wa Mazingira.

Miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika Kikao Kazi hicho ni Wizara ya Maji, Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu Ardhi, EWURA, SNV na WaterAid, pamoja na wadau wengine wa Sekta ya Maji na Usafi wa Mazingira.

Kikao hicho ni sehemu ya hatua za awali za maandalizi ya Mkakati na kinatarajiwa kujenga uelewa wa pamoja kuhusu msingi wa kisera na kisheria, hali ya sasa ya menejimenti ya tope kinyesi vijijini, majukumu ya wadau, mbinu za maandalizi ya Mkakati pamoja na mpango wa utekelezaji wa kazi ya National Task Force.

Kupitia mchakato huo, RUWASA inalenga kuhakikisha kuwa Mkakati utakaoandaliwa unatoa mwelekeo wa kitaifa na mfumo unaotekelezeka wa menejimenti salama na endelevu ya tope kinyesi katika maeneo ya vijijini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira na kulinda afya ya jamii na mazingira.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com